Mwanasiasa mkongwe, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ametangaza rasmi kuachana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) alichokitumikia kwa zaidi ya miaka 60 akianza na TANU.

 Mzee Kingunge ameweka wazi uamuzi wake huo leo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Mzee Kingunge ameeleza kuwa hatajiunga na chama chochote cha siasa ingawa amesema anaunga mkono vuguvugu la wananchi wanaohitaji mabadiliko nchini kupitia vyama vya upinzani.

 Ameeleza kuwa CCM iliacha njia na kwenda kinyume na katiba ya chama wakati wa mchakato wa kumchagua mgombea urais wa mwaka huu na kwamba viongozi wa chama hicho walivunja katiba kwa maslahi yao binafsi.

Hii ni sehemu ya hotuba ya Mzee Kingunge:

“Kwa kuwa viongozi wameamua kukibinafsisha chama, sijui ni kwa maslahi ya nani. Vijana wanatumiwa kudhalilisha watu wazima. Mavuvuzela wanaajiriwa kwa ajili ya kuwatukana tu watu. Kwa hiyo mimi nasema mimi sikubaliani. Hicho sio chama tulichoshirikiana kukijenga. Hiki ni chama kingine.

 “Na kwa hiyo mimi kuanzia leo, naachana na Chama Cha Mapinduzi. Kwa sababu siwezi kuhimili chama kinachoendeshwa bila kuheshimu Katiba. Kwa sababu katiba ndio inayotuunganisha sisi sote.

 “Sasa nasema kuanzia sasa, mimi najitoa kwenye Chama Cha Mapinduzi. Najua uwamuzi wangu, utawasumbua baadhi ya ndugu zangu, rafiki zangu, makada wenzangu, wazee wenzangu ambao pengine tunawasiliana mara kwa mara. Hata vijana wengi. Lakini ni uamuzi ambao lazima niufanye kwa sababu vinginevyo mimi nitajisaliti mwenyewe. Nimehusika katika kuweka misingi ya chama chetu kwa sababu tuliamini ndio misingi sawasawa.

 “Nimeshiriki kuhakikisha kwamba ndani ya chama chetu kunakuwa na demokrasia. Sasa demokrasia imepigwa mateke. Halafu wakuu wa chama wanasimama mbele ya hadhara na kusema kuwa taratibu zote zimepitishwa.

 “Pili, sikusudii kujiunga na chama chochote, na nina sababu. Mimi nimekuwa mwanaharakati ndani ya vyama, TANU na sasa CCM kwa pamoja kwa miaka 61. Nimekuwa mwanaharakati wa kutafuta uhuru mpaka tumeupata na mwanaharakati wa kujenga Tanzania mpya. Nadhani miaka 61 imetosha kuwa mwanaharakati. Sasa mimi nadhani ukiingia ndani ya chama unapaswa kuheshimu Katiba na kuwaheshimu wenzako.

 “La tatu, mimi ni raia tena raia huru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nina haki zangu, haki za kisiasa na za kijamii. Kwa hiyo, nitaendelea kuwa na misimamo kuhusiana na masuala ya nchi yangu. Hii ni nchi yangu, na kwa bahati nzuri nimeipigania iwe huru. Sasa katika hali ya sasa, lazima nitoe msimamo wangu. Hali ya sasa unaweza kusema ina makundi mawili, kundi moja linasema ‘kidumu chama Tawala’, maana yake hakuna mabadiliko. Kundi jingine, linasema ‘Tunataka Mabadiliko katika nchi yetu’, sasa sitaki kusema kundi lipi kubwa lakini nasema hali iko hivyo.

“Lakini kwa jinsi navyotazama, vijana wanataka mabadiliko, walio wengi. Ukiondoa kale kakundi ka viongozi wa UVCCM, wale vijana wangu. Lakini vijana wengi wanataka mabadiliko, nasikia hiyo. Kila napopita nasikia hivyo.

 “Najua vijana wengi wanataka mabadiliko, wakulima, wavuvi, kina mama, wachimba migodi wadogowadodo, najua wengi wao wanataka mabadiliko. Wanafunzi hasa wale wa sekondari ya juu na wa vyuo na vyuo vikuu walio wengi wanataka mabadiliko. Najua na wasomi wa nchi hii, walio wengi wanataka mabadiliko. Nilisema siku moja ITV, zamani kidogo kabla hatujaingia kwenye harakati hizi. Waliniuliza nani anafaa kugombea urais, nilisema mimi ntamuunga mkono Yule ambaye zipo dalili zote wananchi wengi wanasema huyu ndiye anayefaa.

 “Na niliwahi kusema siku moja kule Arusha nikiwa na Lowassa. Mwalimu anasema, katika harakati zote hizi za kutafuta urais, ulizeni wananchi wanataka nini. Msikae kwenye ofisi zenu mkadhani mnamtafuta katibu kata. Mnamtafuta rais wa nchi.

“Lazima mumtafute mgombea ambaye anakubalika ndani ya CCM na nje ya CCM.

 “Na sasa katika huu upande, mimi niko upande wa mabadiliko. Tena mabadilko yanahitajika sasa, na yamechelewa. Kwa nini nasema hivyo. Kama akina mama, wakulima, wafugaji, wavuvi, wazee, wasomi, walio wengi wanataka mabadiliko, lazima wana sababu. Sasa mimi nasema niko kwenye upande wa mabadiliko kwa sababu za wazi.

“La kwanza, kwanza katika historia zetu, sisi katika Tanu, Afro Shirazi na CCM tulikuwa katika upande wa mabadiliko. Kupata uhuru, mapinduzi, tukaamua tuungane tupate mabadiliko. Nchi ziliugana na kila chama kikabaki katika nchi yake, mwaka 1977, tukakubaliana kuiua Tanu, kuiua Afro Shirazi tupate CCM, ni Mabadiliko.

 “Mwaka 1992, mfumo wa vyama vingi. Tena sisi wenyewe, kwenye mkuano wetu, mwaka 1990 Februari, Mwalimu akasema ‘hivi jamani sisi kwanini tusikubaliane kuwa na vyama vingi? Baada ya kujadiliana siku nzima, tukakubaliana kwenda kwa wananchi kuwauliza. Sisi wewenyewe… wananchi wakasema wanataka chama kimoja.

 “Lakini sisi wenyewe chini ya uongozi wa Ali Hassan Mwinyi, lakini tukakubaliana hapana, pamoja na kwamba wengi wanataka tubaki hapa, lakini ni kwa maslahi ya Taifa tunatakiwa tulete mabadiliko. Issue ikawa sasa tunafanyaje?

 “Kwa hiyo nasema kwa ufupi, CCM, Tanu na Afro Shirazi siku zote walikuwa katika upande wa Mabadiliko. Isipokuwa CCM ya sasa. Ukiona watu ambao wanabadilisha hadi kibwagizo cha Chama. Sisi tunasema ‘Kidumu Cha Mapinduzi, sisi tunasema Kidumu. Lakini sasa wanataka tusema ‘Kidumu Chama cha Tawala’. Sasa kama mnataka mjiite ‘Chama Tawala’

 “Sasa kauli zinazotoka hivi sasa, wapinzani hawawezi kushinda, sasa nyie mnajuaje kama hawatashinda. Sasa mimi nasema ukiritimba wa chama kimoja umefikia mwisho. Tunajua madaraka hulevya, nyie mnajua msemo wa kiingereza, “Madaraka hulevya, Power corrupts.

 “Kilichokuwa chama change cha CCM, tatizo lake ni kwamba, baada ya kukaa madarakani kwa miaka mingi, hakiwezi kuleta jipya. Pamoja na ahadi za Magufuli, sasa yeye mwenyewe kapewa nafasi ya kugombea baada ya kuvunjwa kwa katiba ya chama ili CCM ibaki madarakani. Chama kinachodumu kwa muda mrefu sana, na nusu karne ni muda mrefu sana. Kwake kila kitu ni sawa, kama jana.

 “Kuongoza nchi ni kama kupanda mlima, unapanda mlima wenzako wanakuvuta. Sasa unafika mahala, pumzi zinakuishia. Huwezi kuendelea mbele, na ukiendelea mbele una maanisha kwamba wananchi wabaki pale ulipo. Na chama cha mapinduzi sasa kimeishiwa pumzi ya kuongoza.

 “Na nitakuambieni, tazama, tatizo la wananchi ni uchumi, ajira, sasa umasikini unaondolewa na uchumi imara, ajira zinapatikana kwa wingi wakati uchumi ni vibrant, umengamka kabisa. Sasa, rais mstaafu Mkapa, alitufanyia kazi nzuri sana. Alitutoa kwenye ukuaji wa uchumi wa asilimia 3 hadi 4, wakati anaacha madaraka akamkabidhi rais Kikwete, uchumi ukawa unakuwa haraka kwa asilimia 7, kwa sababu wanatoka mbali kwa uchumi kukua kutoka kwa Mkapa. Sasa tazama, rais Kikwete alipokea madaraka kwa Mkapa uchumi unakuwa kwa asilimia saba, baada ya miaka 10 uchumi unakuwa karibu na asilimia 7.

 “Tazama miaka kumi hii tunapiga mark time, na kupiga mark time ni kurudi nyuma. Wakati uchumi unakuwa kwa asilimia 7 idadi ya watu ilikuwa ngapi, na sasa imekuwa takribani watu milioni 10.

“Ni jambo la ajabu kuona hata bei ya sukari sasa ni yakuruka. Mkapa alituacha na sukari inauzwa shilingi 600, hivi sasa ni 200 hadi 2500. Nini tatizo? Ni ‘Pumzi’. Kupanda mlima kunataka pumzi, kuongoza watu kunataka pumzi.

 “Mwaka 2005 tulianza na ‘Maisha Bora kwa kila mtanzania’ lakini sasa hivi hatusemi tena hivyo. Kwanini, hatuwezi, tutagombana na wananchi. Kwa sababu mabadiliko hayaepukiki, tunatakiwa tupate watu wapya, pumzi mpya. Sasa mnataka mbaki nyie tu.

 “Kwa hiyo mimi nasema mabadiliko ni lazima, na mimi sitaki chama changu hiki cha zamani kisivunjike. Mimi nataka kikae benchi kidogo. Kipate nafasi ya kujitathmini. Chama hiki sasa hivi hata kimeacha kujadili issues.

 “Kwa hiyo mabadiliko yanahitajika ili kuwaondoa watu kwenye umasikini. Watu wa nje wataalam wanasema, ili uchumi uimarike, angalau uchumi wa nchi ukue angalau kwa asilimia 10. Sasa kutoka asilimia 7 hadi 10 sio mbali sana. Lakini tunapiga mark time. Miaka mitano inawezekana.

 “Sasa nasema, tunahitaji mabadiliko. Yako mambo yanayokera watu, sio tu kilimo, ajira, na kila nchi inatatua matatizo ya ajira kulingana na mazingira yao. Huko kwenye CCM tuna sera nzuri sana. Mimi nimekuwa ndio mwenyekiti wa ilani zote za uchaguzi isipokuwa moja, tangu mwaka 1990. Na nimekuwa mwenyekiti wa partsan. Mwaka 2000 tuliunda sera ya kuwawezesha wananchi kiuchumi. Tukitaka nchi ikue, tunatakiwa kuwawezesha wananchi kimaarifa, kitaalam na kiuchumi.

 “Mnaandika kwenye guidline, hakuna siku moja mnakaa mnajadili suala la kuwawezesha wananchi kiuchumi. Sasa mnataka mtu apate ajira, mnataka ajiajili, ili awe na uwezo wa kujiajiri

 “Sasa wanaotaka kujidanganya kwamba Magufuli ataleta mabadiliko, haya… fikra mpya ziwepo. Washike dola watu wapya. Na CCM kama chama cha upinzani, kisaidie kutoa uzoefu. Na CCM kulazimisha kuwa lazima tuwe madarakani, mtajilaumu wenyewe.

 “Akina mama mnaambiwa kuwa kuna mkakati umeanzishwa, uko Marekani. Mkitaka mambo yabadilike lazima tuanzie hapa. Watu wako wanalima, mnatakiwa kuwawezesha wakulima huko.

 “Na sasa hivi kuna matabaka, wasio nacho na walionacho. Chama chetu kile ni cha kijamaa. Wakiingia madarakani, unaona majumba yanaanza kufumua majumba, watoto wanawili tu kupita kiasi.

 “Tufike mahala tujenge uchumi endelevu unaotegemea nchi yenyewe.

“Nimalizie, nimezungumza kidogo. Kwanza nataka vijana mjue bado mimi ni ‘mwendo mdundo, hamna shinda’. Lakini niseme tumefika mahala pagumu. Nguvu ya kupinga mabadiliko ni kubwa sana. Lakini kwa utafiti wa mzee kama mimimi, nguvu za kuleta mabadiliko ni kubwa zaidi. Kwa hiyo mimi nataka watu wajiamini zaidi, wakisubiri tarehe 25 mwenzi huu wa Oktoba.

 “Mimi nataka niwashukuru ninyi, na wananchi ambao watapata kusikiliza maneno yangu, nawashukuru sana.”

 

 

Chadema wamgomea tena Jaji Lubuva, Macho Yote Kituo Cha Kura
Lowassa Amng’ang’ania Mgombea Ubunge Wa Monduli CCM