Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Mulamu Nghambi, amewataka Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo kupuuza yanayosemwa Mitandao kuhusu Usajili wa Mshambuliaji Mzawa Habib Kyombo.

Simba SC ilimtambulisha Kyombo Jumamosi (Julai 09), akiwa mchezaji wa kwanza kuanikwa hadharani na wababe hao wa Msimbazi katika kipindi hiki cha Dirisha la Usajili wa kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Mshambuliaji huyo amejiunga Simba SC akitokea Mbeya Kwanza baada ya awali kusaini pia Singida Big Stars, huku baadhi ya Mashabiki wa klabu hiyo wakiwaka kupitia mitandao ya kijamii, lakini Mulamu alifichua dili la mchezaji huo na sintofahamu yake, huku akiwatuliza Mashabiki hao.

Mulamu amesema Uongozi wa Simba kupitia kamati maalum ya Usajili imefanya maamuzi sahihi ya kumsajili Mshambuliaji huyo mzawa, wala haikakurupuka ama kubahatisha kama wadau wengi wanaopinga kutoa sababu zao ambazo hazina mashiko.

 “Wasichokijua watu wengi Kyombo ni mchezaji aliyewahi kucheza Simba B, hivyo amerejea nyumbani, ndio maana yeye akaomba avunje mkataba wake na SBS aliposaini hapo awali,” amesema Mulamu

“Jambo lingine hakusaini sehemu mbili ila baada ya kuona viongozi wa Simba SC wamemfuata ndipo alipoamua kwenda kuuvunja mkataba wake mwenyewe na Singida Big Stars alikosaini miaka miwili ndio maana suala lake limeisha kwa amani.”

Mbali na hilo, Mulamu amewatoa hofu Mashabiki na Wanachama wa Simba SC na kusisitiza kuna silaha watazishusha ambazo zitakosha mioyo yao, hivyo wasihangaike wala kupata presha na kile kinachoendelea kufanywa na wapinzani wao kwani hawasajili kwa mihemko.

“Simba SC ni levo nyingine na tulishaachana na tabia za kushindania wachezaji, tuna watu wanaofanya skauti za maana kulingana na mahitaji ya timu yetu, mashabiki wetu watulie na waunge mkono juhudi ambazo zinazofanywa na viongozi wao,” amesema Mulamu.

Kyombo aliwahi kung’ara na Mbao FC na Singida United zilizoshuka Daraja, kisha alitimkia Afrika Kusini na aliporejea alijiunga na Mbeya Kwanza FC iliyoshuka pia msimu huu na katika michezo 12 aliyoichezea alifunga mabao sita.

Wakati huo huo Simba SC leo Jumatatu (Julai 11) imemtambulisha rasmi Kiungo Nassoro Kapama kwa Mashabiki na Wanachama wake, kupitia Simba APP na Kurasa za Mitandao ya Kijamii za Klabu hiyo.

Simba SC imemtambulisha Kiungo huyo wa zamani wa klabu za Ndanda FC na Kagera Sugar kwa kuandika ujumbe katika kurasa zake za Mitandao ya Kijamii: “Kipaji kikubwa kutoka kwenye ardhi iliyobarikiwa ya Tanzania kuja kuongeza nguvu kwenye kikosi chetu. Nassoro Kapama ni ??????”

Polisi, TCRA kuimarisha usalama wa mtumiaji mawasiliano
Binti wa Rais ataka uchunguzi kifo cha baba yake