Jeshi la Polisi, limesisitiza kuimairisha zaidi ushirikiano baina yake na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kuhakikisha watumiaji wa huduma za mawasiliano wanakuwa salama.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro wakati alipotembelea banda la TCRA katika viwanja vya maonesho ya sabasaba jijini Dar es salaam.

“Ukifanya uhalifu mtandaoni utaadhirika na utakamatwa, hivyo nawaasa watanzania tujiepushe na utapeli mtandaoni” ameonya IGP Sirro.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro akisaini Kitabu cha Wageni katika Banda la Maonesho la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA katika viwanja vya Maonesho ya Biashara SabaSaba jijini Dar es salaam.

Hata hivyo, ametoa wito kwa TCRA kuendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano, kwa madai kuwa ndiyo njia sahihi ya kupunguza tatizo la uhalifu wa mitandao.

“Suala muhimu ambalo ningependa kuwashauri TCRA ni kwamba tuendelee kutoa elimu, tuna watu wanatenda uhalifu bila kujua kwamba ni uhalifu kwenye mtandao, hivyo elimu ni jambo la msingi sana,” amesema Sirro.

Afisa Mwandamizi Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Sauli Mwakyanjala, amemuambia IGP Sirro kuwa wanaendelea na jitihada ya kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi na salama ya huduma za Mawasiliano.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro akihojiwa na Afisa Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Sauli Mwakyanjala kwenye banda la maonesho SabaSaba jijini Dar es salaam.

Amesema, TCRA imeweka utaratibu wa watumiaji huduma za Mawasiliano ya simu kutoa taarifa ya uhalifu kupitia namba maalum, sambamba na kuwataka watumiaji wote wa simu kuhakiki laini zao simu zilizosajiliwa kwa namba za kitambulisho cha Taifa (NIDA).

“TCRA tuna utaratibu unaomwezesha mtumiaji huduma za Mawasiliano ya simu kutoa taarifa ikiwa atapokea ujumbe au simu ya utapeli kwa kutuma namba ya tapeli kwenda namba 15040, utaratibu huu tunautekeleza kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi,” amefafanua Semu.

Aidha, amesema watumiaji wa huduma za mawasiliano wanapaswa kuhakiki usajili wa laini zao za simu kwa kubonyeza *106#, ili kuona na kufuta namba sizizotambuliwa.

Majaliwa aagiza fedha za ndani zitumike katika miradi
Kiongozi Simba SC afunguka usajili wa Habib Kyombo