Kiongozi wa Kikundi cha Wapiganaji wa Boko Haram, Abubakar Shekau ameonekana kwenye video mpya muda mfupi mara baada ya Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari kutamka hadharani kuwa kikundi hicho kimesambaratishwa.
Video hiyo ni ya kwanza kutolewa na Shekau baada ya kukaa kimya cha miezi kadhaa iliyopita, huku akiwa ni miongoni mwa viongozi wanaosakwa kwa hamu.
Aidha, Kiongozi huyo amekiri kundi lake kuhusika katika matukio ya hivi karibuni nchini Nigeria katika maeneo ya kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo ikiwemo lile lililotukia siku ya sikukuu ya Christimas katika kijiji cha Molai nje ya jiji la Maiduguri, mji mkuu wa Jimbo la Borno.
Hata hivyo, mpaka sasa serikali ya Nigeria haijatoa tamko lolote kuhusu mkanda huo wa video na ujumbe uliomo ndani yake, ingawa jeshi la Nigeria limekiri kuwafukuza waasi kutoka katika ngome zao kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo.