Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeeleza kuwa pindi nafasi za ajira zitakapotoka serikalini itatoa kipaumbele cha kuongeza wauguzi hospitalini kwa kuwa inatambua upungufu uliopo wa wauguzi kwenye hospitali za rufaa za mikoa .
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka wizara ya afya Bi. Ziada Sellah wakati akiongea na wauguzi na wakunga kwenye Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara .
Licha ya upungufu wa wauguzi katika hospitali hiyo Mkurugenzi huyo pia amewataka wauguzi hospitalini hapo kuzingatia maadili ya kazi na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wagonjwa, ili wagonjwa waweze kupata ahueni kwa kupatiwa huduma nzuri kutoka kwa wauguzi.
Imetajwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara inakabiliwa na upungufu wa wauguzi 200, ambao ni zaidi ya asilimia 60% ya mahitaji.
Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga yupo kwenye ziara ya kikazi ya kukagua huduma za Uuguzi katika hospitali za Rufaa za mkoa ya Singida,Manyara,Arusha, Kilimanjaro na Arusha pamoja na hospitali maalum na kanda ili kusikiliza changamoto zinazoikabili kada hiyo ya wauguzi na kuzipatia ufumbuzi ili wauguzi waweze kufanya kazi zao katika mazingira rafiki.