Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini umepewa changamoto ya kuhakikisha kuwa unatekeleza Diplomasia ya Uchumi pamoja na Diplomasia ya Siasa iliyopo ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM (2020-2025) ili kuleta manufaa ya Taifa.
Changamoto hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge wakati alipotembelea Ubalozi huo jijini Pretoria nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kujionea utendaji kazi wa Ubalozi na mali za Serikali nchini humo.
“Nawapongeza kwa utendaji kazi wenu na nawasihi muendelee kujituma katika kazi (proactive) katika kuwapata wawekezaji na kutengeneza kuwa ni sehemu ya mfumo wa kuleta mabadiliko ambayo Serikali imeyapanga kupitia Ilani ya CCM ya 2020-2025” amesema Balozi Ibuge.
Balozi Ibuge pia amepongeza utendaji wa Ubalozi huo ambao pamoja na Afrika Kusini, unaiwakilisha Tanzania katika Ufalme wa Lesotho, Jamhuri ya Botswana, Jamhuri ya Namibia na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kadhalika Balozi Ibuge alipokea changamoto mbalimbali zinazoikumba Ubalozi huo na kuahidi kuzifanyia kazi ili kuongeza tija na ufanisi wa Ubalozi.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania Nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Gaudence Milanzi amemueleza Balozi Ibuge mafaniko mbalimbali ya Ubalozi katika kutekeleza diplomasia ya uchumi na siasa nchini Afrika Kusini, miongoni mwa mafanikio hayo ikiwa ni kuenezwa kwa lugha ya Kiswahili.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Afrika Kusini tutasaini mkataba wa kutumika kwa lugha ya Kiswahili katika shule za Afrika Kusini mwezi wa Machi 2021”amesema Balozi Milanzi.
Pamoja na mambo mengine Balozi Milanzi ameahidi kusimamia sera ya Diplomasia ya uchumi pamoja na Diplomasia ya siasa kwa kuhakikisha kuwa ubalozi utaendelea kuwasiliana na wawekezaji mbalimbali wa kuwekeza nchini Tanzania katika sekta za Biashara, Madini na Mawasiliano.