Baraza la Mawaziri nchini Uganda limeidhinisha utekelezwaji wa agizo la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) la kukubali Kiswahili kuwa lugha rasmi.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda agizo hilo lilitolewa Juni 10, 2022 wakati wa kufunga mazoezi ya vikosi vya jeshi la nchi wanachama zinazojumuisha Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Burundi, Tanzania, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Waziri wa Mawasiliano wa Uganda Chris Baryomunsi amesema agizo hilo linalenga kurahisisha mawasiliano na kukuza utamaduni, biashara na umoja miongoni mwa nchi wanachama wa EAC.

Kufuatia uamuzi huo wa Uganda, Baryomunsi, alisema kuwa lugha hiyo ni ya lazima na itatumika kutahiniwa na hivyo sasa itafundishwa katika shule za msingi na sekondari.

“Ilikubaliwa zaidi kwamba programu za mafunzo kwa Bunge, Baraza la Mawaziri na vyombo vya habari zianzishwe,” alinukuliwa waziri Baryomunsi.

Uganda sasa inaungana na Tanzania na Kenya katika kuifanya lugha hiyo kuwa rasmi, ingawa si rasmi, lugha hiyo pia inazungumzwa katika sehemu za Burundi, Rwanda na DR Congo.

Mnamo 2021, nchi wanachama wa UNESCO zilipokutana jijini Paris, Ufaransa, ziliteua Julai 7 kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Ulimwenguni.

Umoja wa Afrika (AU) umepitisha Kiswahili kama lugha yake rasmi ya kazi mnamo Februari 2022 wakati wa kikao cha kawaida cha 35 cha umoja huo mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Rais Samia aipongeza Serengeti Girls, Wizara Ya Michezo
Rais Samia: Serengeti Girls watungiwe nyimbo za hamasa