Kusimama kwa Ligi Kuu Tanzania Bara ili kupisha Michezo ya Kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ kumetajwa kama faida kwa ajili ya maandalizi ya kikosi cha Kagera Sugar.

Timu hiyo ya Mkoani Kagera ilianza vibaya msimu huu 2022/23 kwa kupoteza 2-1 dhidi ya Azam FC, kisha ikaambulia kichapo cha pili 2-0 mbele ya Simba SC, michezo yote ikichezwa Dar es salaam.

Kocha Mkuu wa Kagera Sugar Francis Baraza amesema mapumziko hayo ya majuma mawili yamemsaidia kujipanga upya, ili kuboresha kikosi chake ambacho kinakabiliwa na majeruhi tangu kuanza kwa msimu huu, hali ambayo anaamini ilisababisha kuwa na mwanzo mbaya.

Amesema muda huo anautumia kikamilifu ili kufanikisha lengo la kufanya vizuri katika michezo inayofuata, hivyo ana uhakika mambo yatakua mazuri Ligi itakaporejea mapema mwezi Septamba.

“Ligi iliposimama nilishukuru. Japo sio wote ambao wataimarika, lakini baadhi yao wameanza kuimarika na kama watakuwa fiti, basi kwenye mechi ya Septemba 6 (dhidi ya Geita Gold) nitakuwa nao,” amesema Baraza.

Amewataja baadhi ya wachezaji wake ambao ni majeruhi kuwa ni David Luhende ambaye aliumia akiwa kwenye timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Dickson Mhilu ambaye ameanza mazoezi kidogo kidogo na Edgar James.

“Huyu aliomba ruhusa aende kwao mara moja baada ya kuona hawezi kubaki Kagera peke yake wakati timu ikiwa imesafiri kwenye michezo yetu ya awali,” amesema.

“Ligi iliposimama kupisha programu za Taifa Stars kwangu ilinisaidia kuboresha kikosi na wale ambao walikuwa hawapati nafasi ya kuanza kujaribu kuwatumia katika mazoezi na michezo kadhaa ya kirafiki ikiwamo ya Kagera Combine.”

Amewataja wengine kuwa ni Mpapi Nasibu ambaye amesema ni mchezaji aliyempa wakati mgumu kuwa nje ya uwanja wakati Ligi Kuu ilipoanza.

Kamati ya Bunge yakutana kujadili miradi EP4R
Kenya: Ruto hakupata asilimia 50+1 ya kura