Wakati Wadau wa Soka la Bongo wakisubiri kutangazwa kwa kocha mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Shirikisho la soka TFF limeweka wazi, namna wanavyoendelea na mchakato huo.
Stars imekuwa haina Kocha tangu alipoondoka Kocha wa muda Hanour Janza, ambaye alirudi nchini kwao Zambia baada ya kupata Dili la kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Klabu ya ZESCO United.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ Oscar Milambo, amesema ni kweli wanaendelea na mchakato wa kumsaka Kocha Mkuu mpya wa Taifa Stars, lakini wanazingatia sifa ya kumpata Kocha, ambaye ataisaidia timu hiyo, pasi na kutoa visingizio vya kukosa wachezaji wasio na misingi ya soka la vijana.
Milambo amesema asilimia kubwa ya makocha waliowahi kuinoa Taifa Stars, wamekuwa na visingizio vya kusema baadhi ya wachezaji wa timu hiyo, wamekuwa hana misingi ya soka la vijana, japo visingizio hivyo huwa hawaviweki wazi wakiwa wanasaini mikataba ya kazi.
“Makocha wengi wakija kufundisha Taifa Stars wamekuwa wakisema wachezaji wetu hawana misingi, sasa huwa tunajiuliza wakati tunakubaliana nao kufanya kazi pamoja hawakulijua hilo? Safari hii tutampa timu kocha anayejua matatizo yetu ili ayatatue” amesema Milambo
Tayari Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amekuwa akihusishwa kubebeshwa jukumu la kuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, lakini hakuna taarifa zozote za kukubali ama kukanusha kutoka kwa viongozi wa TFF.
Pia viongozi wa Young Africans ambao wana haki ya kimkataba na Kocha huyo, nao wamekuwa kimya, licha ya Kocha huyo kutoka nchini Tunisia kuendelea kuhusishwa na mpango wa kupewa jukumu la kitaifa.