Klabu ya Azam FC imetangaza kuwa, inasubiri makocha wake raia wa Hispania, Zeben Hernandez na Jonas Garcia warejee nchini ndiyo waanze kuangalia namna ya kuwakata baadhi ya wachezaji wanaoona hawatawafaa kwa msimu ujao.
Kumekuwa na taarifa kwamba, Azam inatarajia kuwapunguza wachezaji kumi kutoka kwenye kikosi chao wakiwemo wale waliomaliza mikataba yao lakini imekuwa ngumu kwa majina ya wachezaji hao kuwekwa hadharani.
Hata hivyo tayari Mkenya, Allan Wanga na Mrundi, Didier Kavumbagu, wapo kwenye orodha hiyo ya watakaoachwa.
Msimu ujao Azam itakuwa na kocha mkuu mpya ambaye ni Hernandez huku Garcia akiwa ni kocha wa viungo, hiyo ni baada ya timu hiyo kuachana na Stewart Hall raia wa Uingereza.
Akizungumzia ishu nzima ya usajili wa klabu hiyo, Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba amesema, Julai Mosi, mwaka huu, wachezaji wao wote wanatarajia kuingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya, na hapo ndipo makocha wao hao watakuwa wamesharejea na kuanza mchakato wa usajili ikiwemo kuwakata baadhi ya wachezaji.
“Kwa sasa hatuwezi kuanza mchakato wa usajili mpaka makocha wetu wale warejee, tunatarajia Julai Mosi watakuwa tayari nchini kwa kuanza kazi kwani siku hiyo pia ndiyo tunaanza kambi yetu ya kujiandaa na msimu mpya.
“Ishu za nani anaachwa na nani anaongezwa, wao ndiyo wataifanya kwani kabla ya kuondoka walipata fursa ya kukiona kikosi na kutambua wachezaji waliokuwa tayari kufanya nao kazi,” alisema Kawemba.
Chanzo: Champion

Video: Zitto Kabwe Kaongea Haya Baada ya Mahojiano na Polisi
Video: Waziri Mpango Ametuletea Mpango wa Maendeleo wa Taifa2016/17, Kayataja Mambo Haya