Kocha Mkuu wa USM Alger ya Algeria, Abdelhak Benchikha amesema hana hofu na kiwango cha Young Africans, lakini wababe hao wa Soka la Tanzania Bara wanapaswa kutegemea mchezo mgumu zaidi ya yote iliyopita, kwani wanahitaji Ubingwa wa Kombe la Shirikisho.

USM Alger itaanzia ugenini Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kucheza mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya wenyeji wao Young Africans Jumapili (Mei 28), huku mchezo wa Mkondo wa Pili ukipangwa kupigwa Juni 03 kwenye Dimba la Omar Hamadi.

Kocha Benchikha amesema anatambua mchezo utakuwa mgumu kwa pande zote mbili, lakini hana budi kuwatahadharisha wenyeji wao kwa kuwaambia mambo hayatakuwa kama walivyozoea katika michezo iliyopita.

Amesema wanatambua Young Africans imekuwa na matokeo mazuri inapocheza nyumbani na imekuwa ikishinda michezo ya ugenini pia, lakini kwa kikosi chake hatakubali hilo lijitokeze kwa urahisi.

Kocha huyo aliyetua USM Alger akitokea RS Berkane ya Morocco mwaka 2022, amesema dhamira yake kuu msimu huu ni kuona kikosi chake kinatwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, na tayari wapo katika ulingo wa kufanikisha mpango huo.

“Wanatakiwa kufahamu kuwa wanakwenda kukutana na timu ya tofauti kuliko walizokutana nazo katika hatua waliyocheza, tunalihitaji hili kombe,tunaheshimu uwezo wao.” amesema Abdelhak Benchikha

USM Alger ilitinga Fainali ya michuano hiyo kwa kuiondoa ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwa jumla ya mabao 2-0 huku Young Africans ikiiondoa Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-1.  

KMC FC yarejea Dar es salaam
Hersi Said: Sikujuwa kama ningekuwa Rais Young Africans