Kikosi cha KMC FC kimelazimika kuvunja kambi mjini Makambako Mkoani Njombe baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons uliotakiwa kuchezwa Mei 24 kusogezwa mbele.

Bodi ya Ligi ilisogeza mbele michezo ya Jumapili ikitoa taarifa rasmi kwamba michezo ambayo ilikuwa ichezwe Mei 26 na 28 za kuhitimisha Ligi Kuu itachezwa Juni 6 na Juni 9.

KMC FC iliondoka jijini Dar es Salaam na kwenda Makambako, Mei 18 ikijiandaa na mchezo dhidi ya Prisons lakini walipopokea taarifa hiyo na wamelazimika kurudi tena jijini.

Afisa Habari wa KMC FC Christina Mwagala amesema baada ya kupokea taarifa hiyo wamelazimika kurudi Dar na kuwapa mapumziko wachezaji wao hao na leo Jumatano mchana watarejea kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Tanzania Prisons.

“Tulienda Makambako mapema ili tuweke kambi pale kwa sababu tunakwenda kucheza Mbeya na hali ya hewa zikiwa zinaendana, kesho Jumanne (leo) ilitakiwa ndio tuanze safari ya kwenda Mbeya lakini tumerudi Dar,” amesema

“Tumetoa mapumziko hadi Jumatano kutokana na uchovu na Jumatano wote watarudi kambini na kufuata ratiba za kocha wetu mkuu kisha ndio tutapanga mipango yetu.”

Mwagala ameongeza akisema: “Ratiba inatakiwa kufatwa kwa sababu ndio ishaamuliwa na watahakikisha wanashinda mechi hizo ili kusalia kwenye Ligi Kuu.”

Dusan Vlahovic kutimkia England 2023/24
Kocha USMA aitumia ujumbe Young Africans