Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imepata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Burundi kwenye mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Urusi 2018 iliyochezewa mjini Bujumbura.

Kwenye mchuano uliochezewa uwanja wa Prince Louis Rwagasore, DR Congo walianza mechi vyema kwa kufunga dakika ya 5 kupitia Yannick Bolasie.

Lakini Burundi walijikakamua na kukomboa bao hilo kupitia Cedric Amissi dakika ya 38 na timu zote mbili zikaenda mapumzikoni zikiwa zimetoshana nguvu.

Kipindi cha pili, vuta nikuvute iliendelea lakini mambo yalifanyika dakika 10 za mwisho.

Burundi ndio waliotangulia kujiweka mbele dakika ya 83 kupitia Amissi tena, lakini mambo yalikuwa bado.

Katika kipindi cha dakika mbili, Ndombe Mubele alifunga mabao mawili, dakika ya 86 na dakika ya 88, na kuwawezesha DR Congo kuondoka na ushindi.

Kwenye mechi nyingine, Guinea walilaza Namibia 1-0, Benin wakakomoa Burkina Faso 2-1 nao Uganda wakatia mkobani ushindi wa bao moja bila dhidi ya Togo.

Farouq Miya alifungia Cranes muda mfupi kabla ya mapumziko. Kipa Dennis Onyango kisha aliokoa mkwaju wa penalti kutoka kwa Mathieu Dossevi.

Kwa kiasi Fulani, Uganda wameweza kulipiza kisasi kushindwa kwao mara mbili na Togo mechi za kufuzu kwa Kombe la Taifa Bingwa Afrika 2015 na Togo.

Mechi ya marudiano itachezewa Kampala Jumapili.

Yafuatayo ndiyo matokeo kamili ya mechi zilizochezwa leo:

Burundi 2-3 Congo DR

Namibia 0-1 Guinea

Benin 2-1 Burkina Faso

Togo 0-1 Uganda

Mvua Yaahirisha Uhondo Wa Soka Buenos Aires
Jose Mourinho Huenda Akanusurika