Wadukuzi kutoka Korea Kaskazini wanadaiwa kuiba mzigo wa mafaili ya kijeshi kutoka Korea Kusini yakiwa na mipango ya kivita hususan mpango wa kumuua kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong-un.
Mbunge wa Korea Kusini, Rhee Cheol-hee amesema kuwa mafaili hayo yalikuwa na taarifa za wizara ya ulinzi ya nchi hiyo yakiwa na taarifa za mpango wa vita uliokuwa unasukwa kwa kushirikiana na Marekani.
Rhee ambaye ni mbunge wa chama tawala cha nchi hiyo na mjumbe wa Kamati ya Ulinzi ya Bunge, ameeleza kuwa mafaili hayo yalikuwa na ukubwa wa 235 gigabytes (GB) na yaliibiwa katika kituo kikuu cha mifumo na taarifa.
Amesema kuwa udukuzi huo ulifanyika mwezi Septemba mwaka jana. Kadhalika, mwezi Mei mwaka huu udukuzi kama huo ulifanyika ambapo tuhuma zilielekezwa tena Korea Kaskazini.
Korea Kaskazini inadaiwa kuwa na timu kubwa ya wadukuzi wanaopatiwa mafunzo katika nchi rafiki ikiwa ni pamoja na China.
Hata hivyo, Korea Kaskazini imekanusha tuhuma hizo ikieleza kuwa mahasimu wao wametunga.
Marekani ambao ni marafiki wa Korea Kusini wamekuwa katika vita baridi ya maneno kuhusu mpango wa Korea Kaskazini wa majaribio ya makombora ya nyuklia.
Rais wa Marekani, Donald Trump ameonya kuwa atachukua hatua kali za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini endapo taifa hilo litaendelea na mpango wake wa makombora ya nyuklia.
Hata hivyo, Kiongozi wa Korea Kaskazini alimjibu Trump akisisitiza kuwa taifa lake litajibu kwa vita kamili endapo litaguswa kwa namna yoyote kijeshi.
Korea Kaskazini imeendelea na majaribio ya makombora yake na imetamba kufanya majaribio ya makombora makubwa na hatari zaidi ambayo wanadai yanaweza kufika katika kona nyingi za dunia ikiwa ni pamoja na sehemu ya ardhi ya Marekani.