Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj DkT. Hussein Ali Mwinyi amesema kwa mara ya kwanza Maadhimisho ya siku ya Mwaka mpya wa Kiislamu, Mwaka 1445 Hijriya kutambuliwa na Serikali kuwa ni siku ya mapumziko.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo katika hafla ya Maadhimisho ya kuukaribisha kuingia mwaka mpya wa Kiislamu yaliyofanyika Msikiti wa Munawar Mfikiwa, Wilaya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba, na kusema Serikali imekubali ombi la Waislamu kuhusu kuiadhimisha siku hiyo kuwa ya mapumziko, kuipa hadhi na kuiongezea hamasa.
“Kwa Mamlaka ya kikatiba chini ya kifungu 6(1)(a)cha Sheria ya Masuala ya Rais wa Zanzibar,Namba:3 ya 2020, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi ameitangaza rasmi kesho Jumatano itakuwa ni siku ya mapumziko Kitaifa Zanzibar,” alisema Rais Mwinyi.
Aidha, Alhajj Dkt. Mwinyi pia ametoa wito kwa Wazazi na Walezi kutimiza wajibu wa malezi ya vijana kuwa na kizazi chema chenye kumjua Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza maarimsho yake na kujiepusha na makatazo katika misingi bora ya maadili kwa mujibu silka na tamaduni za dini.