Beki kutoka nchini Ghana na klabu ya Young Africans, Lamine Moro ameitwa na Uongozi wa juu wa Klabu hiyo ili kusikiliza shauri lake la Utovu wa nidhamu lililowasilishwa kwa Uongozi na Benchi la Ufundi.
Lamine ambaye ni nahodha wa kikosi cha Young Africans, alilazimika kurejeshwa jijini Dar es salaam, baada ya kudaiwa kuonesha utovu wa nidhamu wakati timu ikiwa kwenye maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo dhidi ya Namungo FC, uliochezwa juma lililopita mkoani Lindi.
Kaimu Katibu Mkuu wa Young Africans, CPA. Haji Mfikirwa amesema, baada ya kupata malalamiko kutoka benchi la ufundi ni muhimu kusikiliza upande wa pili ili kutoa maamuzi ya haki kwa pande zote.
“Benchi la Ufundi limelalamika, na kwa nafasi yao walichukua hatua za awali zilizoko kwenye Mamlaka yao, kwa kuwa wamelileta kwa Uongozi, sasa ni muhimu Sana tukamsikiliza mlalamikiwa kisha kutoa maamuzi kama klabu,” amesema CPA. Haji.
Amesema suala la Lamine ni la kinidhamu lililoanzia kwenye bechi la ufundi na halihusiani chochote na kuidai klabu na kwamba nyota huyo hana deni lolote analoidai klabu kwa mujibu wa makubaliano.
“Lamine hadai chochote, hivyo taarifa za kwamba anaidai klabu ni za uzushi na zipuuzwe, suala lake limetokana na masuala ya benchi la ufundi, na tutalitolea taarifa baada ya kamati kukaa na kusikiliza,” amesema.
Kutokana na hali hiyo Lamine Moro ameendelea kukosekana kwenye kikosi cha Young Afrucans kwa michezo miwili dhidi ya Namungo FC na JKT Tanzania, huku kukiwa hakuna dalili zozote za kujiunga na wenzake katika maandalizi ya mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Mwadui FC, utakaochezwa mapema juma lijalo.