Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani mauaji ya mtangazaji wa televisheni ya ITV wa kipindi cha Jarida la Wanawake, Blandina Sembu na kutaka wahusika wa tukio hilo kukamatwa na kuchukuliwa hatua.
Hayo yamesemwa na mkurugenzi mtendaji wa LHRC, Anna Henga kwa mujibu wa gazeti mwananchi ameeleza kuwa ipo haja kwa polisi kufanya uchunguzi huo haraka ili hatua zilichukuliwe kwa wahusika.
Mwili wa Blandina ulikutwa pembezoni mwa barabara mita chache kutoka ilipo baa ya Maryland iliyopo eneo la Mwenge, njia panda ya kuelekea ITV mkoani Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoa wa kipolisi Kinondoni, Ramadhan Kingai, mwili huo ulitupwa usiku wa Machi 27, 2021 saa 5:30 usiku kutoka katika gari aina ya Toyota Noah ambalo namba zake hazikujulikana.
“Tunatambua kwamba ibara ya 14 ya katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania 1977 inatamka bayana kwamba kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha kutoka kwa jamii yake.”
“Kinachosikitisha hatupati taarifa za kina kuhusu kifo chake maana maneno mengi yanazungumziwa kuhusu tukio hilo,” amesema Anna.