Tanzania imepata taarifa nzuri kutoka Marekani, ambapo usiku wa kuamkia leo Omary Tambwe maarufu kama Lil Ommy ametangazwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Mtangazaji Bora Afrika katika Tuzo za African Entertainment Awards – USA (AEAUSA) tuzo ambayo ni ya kwanza Tanzania kuipata kwenye kipengele hicho.
Kwa mujibu wa waandaaji wa tuzo hizo zilizofanyika jijini New York nchini Marekani, Lil Ommy amefanikiwa kuwapenya washindani wake katika kipengele cha Best Host. Kadhalika, mwimbaji Nandy naye ameiwakilisha vyema Tanzania akinyakua tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kike Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini.
Wakali kutoka WCB nao wameibuka vinara kwenye tuzo hizo, Diamond akishinda tuzo ya Wimbo Bora wa Kushirikiana (‘Baila’, akimshirikisha Ft Miri Ben Ari) na Ray Vanny akishinda tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kiume Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini.
Kupitia mtandao wa Twitter, Mtangazaji huyo ambaye hivi karibuni alifanya mahojiano maalum na Dar24 kuhusu ushiriki wake kwenye tuzo hizo, amewashukuru mashabiki kwa kumpigia kura na kumfanikisha kushinda.
“Asante sana kila mmoja kwa kura zenu na sapoti yenu ya kutosha, ASANTE SANA MASHABIKI wooote kwa kura na nguvu yenu imeonekana… Love always win…. Tumeweza kuichukua tuzo ya Mtangazaji Bora wa Mwaka Afrika,” ameandika Lil Ommy.
Hata hivyo, hiyo ni tuzo ya kwanza kuinyakua kati ya Tuzo tatu alizotajwa kuwania mwaka huu akiwa Mtanzania pekee kwenye kipengele hicho.
Anasubiri majibu ya tuzo kama hiyo kwenye Tuzo za AFRIMMA zitakazofanyika Oktoba 26, 2019, Dallas nchini Marekani. Katika tuzo hizo zinazowahusisha pia wanamuziki, kwenye tasnia ya habari mbali na Lil Ommy, kutoka Tanzania pia DJ D Ommy wa Clouds Fm atakuwa anawania tuzo ya DJ Bora Afrika, tuzo aliyoinyakua mwaka 2016.
Wasanii wengi pia watahusika kwenye tuzo za AFRIMMA mwaka huu ingawa wasanii wa hip hop wamekosa nafasi hiyo.
Lil Ommy pia atawania tuzo ya Mtangazaji Bora kwenye tuzo za StarQT Awards zitakazotolewa usiku huohuo nchini Afrika Kusini.
Dar24 inawapongeza kwa kupeperusha vyema bendera ya Tanzania na tunaamini tuzo nyingine zitakazofanyika mwezi huu zitakuja pia nyumbani.
-
Hawa ‘Diamond pekee aliamini nitakuwa sawa nimechora Tattoo kumshukuru”
-
Kwa nini watu huchukua uamuzi wa hujiua? ”Kuishi ni kuteseka”