Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amesema kuwa amemuandikia barua Katibu wa Bunge akidai malipo ya mshahara wake pamoja na posho za tangu Januari mwaka huu.
Maelezo hayo ya Lissu yanakuja kufuatia uamuzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kutangaza kusitisha mshahara wa mbunge huyo kwani hajawasilisha taarifa ya maendeleo ya matibabu yake huku akionekana akifanya ziara katika nchi mbalimbali.
Lissu amesema kuwa katika barua yake iliyowasilishwa na mawakili wake wakiongozwa na John Mallya, ameitaka Ofisi ya Bunge kumlipa mshahara wake ndani ya kipindi cha siku 14 vinginevyo atafungua shauri mahakamani.
“Mawakili wangu walimuandikia barua katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai kumtaka kulipa posho na stahili zangu za kibunge tangu Januari mwaka huu. Barua hiyo ilimpa siku 14 kutekeleza madai yangu vinginevyo tutafungua madai Mahakama Kuu kudai haki yangu,” Mwananchi wamemkariri Lissu.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge alipoulizwa alisema bado hajapata barua yoyote kutoka kwa Lissu au mawakili wake.
Wakili wa Lissu, Mallya alieleza kuwa walituma barua hiyo kwa njia ya dispatch pamoja na njia ya EMS katika Ofisi za Bunge na kwamba iliandikwa Machi 18 mwaka huu.
Lissu ambaye anatibiwa nchini Ubelgiji kufuatia tukio la kushambuliwa kwa risasi Septemba 2017 jijini Dodoma, hivi karibuni alifanyiwa upasuaji wa 24 na amesema anaendelea vizuri akifanya mazoezi ya kukunja goti na kunyoosha mkono wake wa kushoto.