Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ameitaka Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha Magereza inajitosheleza kwa chakula kupitia miradi mbalimbali inayomilikiwa na Jeshi hilo.

Waziri Lugola aliizindua Bodi hiyo Mei 30, 2019, na kutoa miezi miwili kwa Wajumbe wa Bodi hiyo, kutembelea miradi mbalimbali ya Jeshi hilo na kumletea taarifa ya awali kuhusu miradi hiyo pamoja na maoni yao.

Akizungumza na Wajumbe wa Bodi hiyo baada ya kupokea taarifa yao, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dodoma, Lugola amesema kuwa taarifa waliyoiwasilisha ameifurahia licha ya kuwa na mapungufu kadhaa ambayo yanahitaji uboreshaji zaidi.

Amesema kuwa Bodi hiyo inawataalam mbaimbali ambao wanaweza wakaleta mabadiliko makubwa ya uzalishaji mali na kuweza kufanikisha Jeshi hilo kujitosheleza kwa chakula kupitia wafungwa mbalimbali waliopo magerezani.

“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri, ila nawataka mfanye kazi zaidi ambayo itatuwezesha kuona mipango mizuri zaidi katika kulisimamia Shirika hili ambalo bodi yake tuliizindua,”amesema Lugola.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga amesema kuwa Bodi yake kwa muda wa miezi miwili ilitembelea mradi wa Ng’ombe wa Nyama Mbigiri, mradi wa Maziwa Kingolwira, mradi wa Uhunzi, mradi wa Kilimo Idete, mradi wa kilimo Kiberege na Mradi wa kilimo Isupilo ambapo Bodi hiyo ilifanya tathmini ya mali zilizopo, mipaka pamoja na historia ya miradi hiyo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu ameitaka Bodi hiyo, ifanye ukaguzi wa kina wa mali za Shirika hilo kiundani zaidi ili taarifa hizo zije kiuhalisia zaidi na kuleta mikakati imara ya mafanikio.

 

Video: Wananchi Kagera wafanya unyama wa kutisha
Wafugaji waangua kilio mbele ya waziri, asitisha operesheni ya kuwaondoa