Kiungo Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Luis Jose Miquissone amesema maisha yake yamebadilika sana, tangu alipojiunga na klabu hiyo, akitokea nchini kwao Msumbiji, Januari 2020.
Miquissone alisajiliwa Simba SC, akitokea UD Songo baada ya kuonesha uwezo mkubwa kisoka timu hizo zilipokuta kwenye mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu wa 2019/20.
Kiungo huyo ambaye pia amewahi kucheza soka Afrika Kusini, amesema alipokua Tanzania alikua na maisha ya kawaida, lakini uwepo wake Simba SC unaendelea kudhihirisha mabadiliko maishani mwake.
“Sio vyema kueleza hapa lakini maisha yangu yamebadilika kutokana na mafanikio ambayo nimeyapata ndani ya Tanzania hata nyumbani kwetu Msumbiji ambapo familia yangu ilipo,” anasema.
“Ndio maana unaona ninapokuwa uwanjani huwa naipigania Simba kwa nguvu zangu zote ili iweze kupata kile ambacho inahitaji kwani natambua mahala iliponitoa.”
“Naamini kwa ushirikiano pamoja na wachezaji wenzangu kwa muda ambao nitakuwa Simba nipo katika timu sahihi ambayo tutapata mafanikio mengi kama tutaweza kuifikisha timu katika malengo yake.”
“Naishi vizuri nikiwa nje ya kambi – kwa maana ya maisha yangu mwenyewe, lakini ndani ya kambi ndio sitamani hata ivunjwe, natamani kuwa na wachezaji wenzangu muda wote,” anasema.
“Tumekuwa tukiishi kwa kupendana, kupeana ushirikiano yaani kama familia moja jambo ambalo awali sikujua kama naweza kukutana nalo maana nilikuwa sifahamu kitu.
“Changamoto huwa zinatokea ambazo lazima tunazipatia suluhisho, kama kipindi cha nyuma nilikuwa sifahamu lugha ya Tanzania (Kiswahili), lakini sasa kwa kiasi fulani naelewa.”
Kuhusu tofauti ya makocha Sven Vanderbroeck na Didier Gomes mchezaji huyo anasema kila mmoja yupo tofauti na mwenzake.
“Unajua kila kocha huwa na mbinu zake katika ufundishaji wake, kwa hiyo wakati wa Sven kuna mambo ya kiufundi ambayo nimeyachota kama ambavyo itakuwa kwa Didier Gomes ambaye tupo naye wakati huu.
“Wote ni makocha bora ndio maana Simba umewachukua ili kuhakikisha tu tunapambana wote kwa pamoja ili kufikia malengo ambayo timu imejiwekea kwa muda wote,” anasema Luis ambaye mashabiki wa Simba wanavutiwa na machachari yake.