Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameweka wazi ahadi ya rushwa ya shilingi bilioni 5 aliyopewa na wafanyabiashara wawili wakubwa.

Lukuvi ameeleza hivi karibuni kuwa wafanyabiashara hao walimuahidi kiasi hicho cha fedha ili awasaidie kufanikisha mpango wao wa kuiuzia ardhi Serikali katika eneo lililopangwa kujengwa Mji Mpya wa kisasa, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

“Kama ukiwa na tamaa huwezi kufanya kazi uliyotumwa. Kuna wakati walikuja wafanyabiashara wawili wakubwa na kutaka wanipe shilingi bilioni 5 ili nikubali kupitisha mradi wao wa mabilioni ya shilingi, na walitangaza kwa rafiki zangu kuwa wangenipa fedha, lakini hapa hawawezi,” Lukuvi anakaririwa na gazeti la Mwananchi lililofanya nae mahojiano maalum hivi karibuni.

Alisema kuwa wafanyabiashara hao walikuwa wamenunua ardhi kutoka kwa wananchi kwa kiasi cha shilingi milioni 5 kwa ekari na baadae walitaka kuiuzia Serikali kwa shilingi milioni 141 kwa ekari ili wavume mabilioni kirahisi.

Waziri Lukuvi alieleza kuwa tayari wamiliki hao walikuwa wamefanikisha mkakati wao lakini alipoingia na kupitia vizuri mikataba alikundua kuna wizi mkubwa na ‘ujaunja’ unaofanyika kutaka kuwatajirisha watu wachache, hivyo aliufuta mpango huo hali iliyopelekea wafanyabiashara hao kuhaha na kuanza kumtafuta.

“Niliwaambia Serikali haiwezi kuwapa fedha hizo na badala yake waendelee kuendeleza ardhi wenyewe kulingana na mradi unavyotaka. Walitaka kujitajirisha kwa ujanja ujanja,” alisema.

“Eti walidai wamekopa benki kwa ajili ya mradi huo. Haiingii akilini mtu tumie shilingi milioni 5 halafu uje uvune mabilioni ya fedha kwa kuvuka pantone tu,” aliongeza.

Lukuvi alieleza kuwa endapo wafanyabiashara hao wangefanikiwa, Serikali ingewalipa zaidi ya shilingi bilioni 84 waliokuwa wanamiliki jumla ya ekari 600, mmoja ekari 200 na mwingine ekari 400.

Ubunifu: Baada ya 'walimu na dadala bure', Makonda aja na mradi wa ‘mtaa wa baa’
Wafanyakazi 597 wa NIDA watimuliwa