Kocha kutoka nchini Zambia George Lwandamina rasmi ametangaza kuwa mkuu wa benchi la ufundi la Azam FC, kwa mkataba wa miaka miwili.
Lwandamina ambaye aliwasili Dar es salaam juzi Jumanne (Desemba 02) usiku, ameajiriwa klabuni hapo akichukua nafasi ya kocha Mromania Aristica Cioaba, aliesitishiwa mkataba wake juma lililopita.
Baada ya kukamilisha taratibu za kujiunga na Azam FC, kocha Lwandamina ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Young Africans, alisema amekuja kufanya kazi baada ya kufikia makubaliano mazuri na uongozi wa timu hiyo.
“Nimefurahi kuja kwa mara nyingine Tanzania, nilikuwapo nikaondoka na sasa nimerudi tena kukinoa kikosi cha Azam FC, imani yangu kuwa pamoja katika mafanikio ambayo yanatarajiwa na uongozi pamoja na mashabiki wa timu hii,” alisema Lwandamina.
Baada ya kukamilika kwa taratibu za kusaini mkataba na klabu hiyo, Lwandamina anatarajiwa kusafiri hadi jijini Mwanza kuungana na kikosi cha Azam FC, ambacho Jumatatu (Desemba 07) kitacheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Gwambina FC.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’, amesema taratibu za kumsafirisha kocha Lwandanmina kuelekea Mwanza zimeshafanywa, na akifika huko ataanza kazi rasmi.
“Kocha ataondoka hapa Dar es salaam na kuelekea Mwanza, taratibu zote za kumsafirisha zimeshakamilika, tunatarajia akifika huko ataanza kazi rasmi akisaidiana na kocha Vivier Bahati, ambaye alikua anakaimu nafasi ya kocha mkuu.” Amesema Popat.
Azam FC ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kucheza michezo 13, iliyowapa alama 26, huku ikifunga mabao 19.