Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad jana alirejea Zanzibar akitokea India alipokwenda kupata matibabu kutokana na kusumbuliwa na maradhi, lakini kuwasili kwake kulikuwa na mshindo wa neno kwa wafuasi wake pamoja na jeshi la polisi.

Maalim Seif alieleza kuwa anaunga mkono tamko lililotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Nassor Ahmed Mazrui lililopelekea kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za uchochezi.

Mwanasiasa huyo ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alieleza kuwa Jeshi la Polisi limegeuka kuwa kibaraka wa Chama Cha Mapinduzi badala ya kutimiza wajibu wao kisheria.

Alisema kuwa Jeshi hilo limekuwa likifumbia macho kundi la watu wanaojulikana kama Mazombi ambao wamekuwa wakiteka na kushambulia wananchi na kuwajeruhi.

“Nasikitika kuona hujuma, watu wakipigwa na kujeruhiwa na mazombi kila kukicha, polisi wapo wanayaona na hakuna aliyeitwa kuhojiwa kwa uchochezi. Sasa haitawezekana na haitakubalika tena…” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais wa CUF katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana alipokelewa katika uwanja wa ndege wa Amani Abeid Karume na viongozi mbalimbali wa chama hicho pamoja na wafuasi wake ambao walimsindikiza hadi nyumbani kwake.

CUF wanapinga kufanyika kwa uchaguzi wa marudio uliopangwa Machi 20 mwaka huu, wakisisitiza kuwa mshindi wa urais wa uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana atangazwe, huku Tume ya Taifa ya Zanzibar (ZEC) ikiweka msimamo kuwa uchaguzi huo ulifutwa kutokana na kuwa na kasoro nyingi.

Hata hivyo, Maalim Seif alipinga madai ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kuhusu dosari zilizopelekea kufutwa kwa uchaguzi huo.

“Nasema sisi hatutambui uchaguzi huo wa marudio maana wameshindwa kututhibitishia ni wapi zilipo hizo dosari za uchaguzi uliokwishafanyika,” alisema.

 

TFF yapinga michezo ya Bahati Nasibu 'Betting'
Nyundo ya TRA kwa Profesa Tibaijuka kuhusu fedha za Escrow yafika ukingoni