Shule nchini Uganda zimefungwa, baada ya Rais Yoweri Museveni kutangaza hatua hiyo kufuatia ongezeko la maambukizi ya Corona nchini humo.
Mikutano ya hadhara pamoja na safari kutoka Wilaya moja kwenda nyingine zimepigwa marufufuku pia kama njia mojawapo ya kudhibiti maambukizi hayo.
Masharti haya mapya yaliyotangazwa na rais Museveni Jumapili usiku, yanaanza kutekelezwa kwa siku 42 zijazo.
Museveni ameeleza kuwa hatua hizi zinahitajika ili kudhibiti maambukizi makubwa ya virusi vya corona nchini humo baada ya maambukizi zaidi ya watu 8000 kuripotiwa wiki mbili zilizopita, ikiwa ndio idadi kubwa kuwahi kuripotiwa tangu kuanza kwa janga hilo nchini humo.
Aidha, Museveni ameonya kuwa hatua zaidi zitachukuliwa iwapo masharti yaliyotangazwa hayatazingatiwa.
Hata kabla ya tangazo hili la rais Museveni, maafisa wa usalama walikuwa wameanza kuwakamata watu wanaokiuka masharti ya kupambana na janga hilo, na wiki moja iliyopita, watu zaidi ya 2000 walikamatwa kwa kukiuka masharti ya kutembea nje kwa muda usiohitajika.