Maafisa wa afya nchini Jamhuri ya Kimokrasia ya Congo DRC, wametangaza rasmi kuzuka tena kwa ugonjwa wa Ebola baada ya kisa kimoja kuthibitishwa kwenye jimbo la Kivu Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo Agosti 24, 2022 na shirika la afya la Umoja wa Mataifa mjini Brazzaville na Kishasa imesema mwanamke mwenye umri wa miaka 46 alifariki dunia Agosti 15, 2022 mjini Beni na alipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya jimbo hilo alikolazwa ambapo baadaye alionyesha dalili za Ebola.
Shirika hilo linasema vituo vyote viwili vya kitaifa vya uchunguzi wa kitabibu Beni na Goma INRB, vimejithibitishia kuwa virusi hivyo ni vya ugonjwa wa Ebola baada ya kufanyia uchunguzi sampuli iliyochukuliwa kwa mgonjwa.
Kwa mujibu wa WHO, uchunguzi umeonyesha kuwa kisa hicho kinahusiana na milipuko miwili iliyodumu kwa muda mrefu nchini humo, ya majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri na kwamba uchunguzi unaendeleaili kubaini hali ya chanjo ya kisa kilichothibitishwa.
Akizungumzia mlipuko huo, mkurugenzi wa WHO kanda ya Africa Dkt. Matshidiso Moeti amesema, “Kujirudia kwa milipuko ya Ebola kunatokea mara nyingi DRC hali ambayo inatia hofu. Hata hivyo mamlaka za afya Kivu Kaskazini zimefanikiwa kuikomesha milipuko kadhaa na kuendeleza utaalam huo bila shaka kutasaidia kuudhibiti mlipuko huu wa sasa haraka.”
Hata hivyo, Wafanyakazi wa WHO na mamlaka za afya DRC wanashirikiana kutafuta chazo cha kusambaa kwa ugonjwa huo, na tayari wamewabaini watu 160 ambao walikutana na marehemu na wako chini ya uangalizi.
WHO inasema, zipo akiba za dozi 1000 za chanjo ya Ebola aina ya rVSV-ZEBOV nchini humo, na dozi 200 kati ya hizo zitapelekwa Beni wiki hii ili kutoa chanjo kwa watu waliokutana na mgonjwa huyo na wale ambao pia waliokutana na watu hao kwa lengo la kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo na kulinda maisha ya watu.
Mlipuko wa mwisho wa ugonjwa huo ulitokea katika mji wa Beni uliopo jimbo la Kivu Kaskazini na ulidhibitiwa ndani ya muda wa miezi miwili ukikoma rasmi Desemba 16, 2021 ambapo wakati huo kulikuwa na visa 11 huku nane kati ya hivyo vikithibitishwa, vitatu vilidhaniwa na ulijumuisha vifo vya watu sita.