Rais John Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Wilson Mbonea Kabwe anayekumbwa na tuhuma za kufanya udanganyifu na kulisababishia jiji hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 3.

Rais Magufuli amechukua uamuzi huo leo wakati akihutubia wananchi katika tukio la uzinduzi wa daraja la Kigamboni ambalo amelibatiza jina la ‘Daraja la Nyerere’, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumuelezea kuhusu udanganyifu huo uliofanywa na Kabwe.

Kabwe

Wilson Kabwe

Makonda alieleza kuwa uchunguzi wa tume yake ulibaini kuwa, Mkurugenzi huyo wa jiji hilo aliruhusu kampuni yenye zabuni ya kutoza ushuru wa mabasi kutumia sheria ya tozo ndogo ya mwaka 2004 katika mkataba wake huku kukiwa na sheria mpya ya mwaka 2009.

Alisema kuwa Kabwe alichukua uamuzi huo kwa makusudi kwa maslahi binafsi kwani sheria ya tozo ndogo ya mwaka 2004 inataka kila basi kutozwa shilingi 4,000 liingiapo katika stendi ya Mabasi ya Kwenda Mikoani ya Ubungo, lakini sheria ya mwaka 2009 inataja tozo ya shilingi 8,000 kwa kila basi.

Baada ya maelezo hayo, Rais Magufuli alitangaza kumsimamisha kazi mara moja Wilson Kabwe. Aliagiza vyombo husika kufanya uchunguzi.

“Kama vyombo hivyo vitamsafisha mimi sitakuwa na neno,” alisema Rais Magufuli huku akisisitiza kuwa ni muda wa watu waliowafanya wananchi kulia kwa muda mrefu, na wao waanze kulia ili wananchi wacheke.

Mama Samia Tunahitaji zaidi Mwenge Sasa, Mtatiro adai Mwenge ni Jipu
ATOLEWA KWENYE NDEGE KWA KUONGEA KIARABU