Kaimu Ofisa Habari wa Manispaa ya Ubungo, Joina Nzali, amesema wameanzisha utaratibu mpya wa kuingia na kadi katika stendi ya kimataifa ya mabasi ya Magufuli, ili kudhibiti upotevu wa mapato kwa abiria wanaoingia katika kituo hicho kilichopo Mbezi Luis.
Matumizi ya kadi hizo, yanaanza leo februari 20,2023 ambapo hatua hiyo imelenga kupunguza changamoto ya foleni hasa wakati asubuhi ambapo kuna kuwa abiria na wasindikizaji wengi katika eneo hilo.
Amesema katika mchakato huo wameshirikiana na Kituo cha Taifa cha Kutunza Kumbukumbu Kimtandao kilichoweka mfumo wa kieletroniki wa kukata na kudhibiti tiketi kwa kutumia milango ya kisasa.
“Mfumo huu utarahisisha huduma kwa wananchi kwa kukidhi mahitaji ya Serikali ya kukusanya mapato kidijitali, kupunguza foleni na kuondoa matumizi ya fedha taslimu kwa watendaji wetu”.
“Kwa upande wa abiria asiyekuwa na kadi, akifika stendi atapatiwa kadi ya kutumia mara moja ambayo akipita itabaki kwenye mlango kwa kumezwa,” amesema Nzali.
Aidha amesema kwa matumizi ya kadi, kila abiria atalazimika kulipia ushuru getini kwa kutumia N- Card hata kama ameshakata tiketi ya basi husika na awali abiria akiwa na tiketi anapita bila kulipa ushuru, lakini hivi sasa atalipia.