Rais John Magufuli ameendelea kukoreza wino kwenye kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ kwa kuwataka Wakuu wa Mikoa kuhakikisha vijana wote wanafanya kazi hata kwa kulazimishwa.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kuwaapisha wakuu wa Mikoa wapya aliowateua wikendi hii.

Alisema kuwa vijana wazembe wanaotaka kufanya kazi huku wakidamka kucheza pool vijiweni wapelekwe kambini wafanye kazi.

“Lakini pia niwaombe wakuu wa mikoa mkasimamie watu wafanye kazi hasa vijana,” alisema Dk. Magufuli. “Haiwezekani vijana leo hii unawakuta saa mbili asubuhi wanacheza Pool table wakati wakina mama wanalima shambani, kama hawataki kufanya kazi kwa kupenda walazimishwe kufanya kazi. Atakayekataa mpelekeni kambini akafanye kazi,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametoa siku 15 kwa Wakurugenzi wa Manispaa zote kuhakikisha kuwa wanaondoa majina ya wafanyakazi hewa wote wanaolipwa mishahara.

Rais Magufuli alisema kuwa anafahamu Dodoma na Singida kuna wafanyakazi hewa 202 hivyo anaamini Wakuu hao wa Mikoa watayafanyia kazi.

Aliwataka wakuu hao wa mikoa kuwachukulia hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwaweka selo viongozi wa ngazi za kata na vijiji wanaowanea wananchi.

“Nyinyi mna mamlaka ya kuwaweka watu ndani( selo) hata masaa 48,wekeni watu ndani ili wajue wananchi wanatakiwa kuheshimiwa. Tusiogope kuchukua maamuzi, nafuu uchukue maamuzi hata kama ni mabaya yatarekebika huko mbele,” alisema Rais Magufuli.

Zanzibar: Baada ya Nyumba ya Kamisha wa Polisi kulipuliwa kwa Bomu, aeleza alivyoathirika
FIGC Wakubali Kumuachia Antonio Conte