Mahakama ya Juu nchini Kenya, imepitisha ushindi wa Rais mteule, William Ruto katika kura ya urais ya mwezi uliopita mara baada ya Raila Odinga kuwasilisha pingamizi la ushindi huo.
Jaji Mkuu wa Mahakama hiyo, Martha Koome amesema Raila na waleta maombi wenzake wameshindwa kuthibitisha kuwa kulikuwa na udanganyifu na uchakachuaji, wakati wa mchakato wa kuelekea uchaguzi, kabla na baada ya kupiga kura.
“Uchaguzi ulikuwa halali na ulifanyika kwa namna huru na wa haki, na hakuna ushahidi wa kuonesha fomu namba 34 ilingiliwa kwa namna yoyote wakati wa kuzipakia kwenye tovuti ya tume ya uchaguzi ,” amesema Jaji Koome katika hukumu aliyoisoma kwa karibu saa mbili.
Akiangazia maswala tisa ya kesi hiyo, Jaji Martha Koome amesema kuwa mshindi wa uchaguzi huo William Ruto alifanikiwa kupita kikwazo cha kura asilimia 50 na moja ya kikatiba ambapo Rais Mteule alitakiwa kuapishwa siku ya kumi na nne baada ya tarehe ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.
Uapisho huo, ungefanyika tu iwapo hakuna ombi lililowasilishwa chini ya Kifungu cha 140, au siku ya saba kufuatia tarehe ambayo Mahakama itatoa uamuzi wa kutangaza uchaguzi kuwa halali, ikiwa ombi lolote limewasilishwa chini ya Kifungu cha 140.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati, alimtangaza Ruto kuwa Rais mteule baada ya kupata kura milioni 7,176,141 (asilimia 50.49) dhidi ya milioni 6,942,930 za Odinga (asilimia 48.85) )Prof George Wajackoyah wa Roots Party akipata kura 61,969 (asilimia 0.44) huku David Mwaure Waihiga wa Agano Party akiibuka wa nne kwa kura 31,987 (asilimia 0.23).