Mahakama Kuu nchini Venezuela imemzuia Kiongozi wa upinzani, Juan Guaidó kutoka nje ya mipaka ya nchi hiyo na kufunga akaunti zake zote za benki.
Hatua hiyo imefikiwa wakati ambapo kuna mgogoro uliotokana na Guaido kujiapisha kuwa Rais wa Mpito wa nchi hiyo, wiki iliyopita.
Mpinzani huyo wa Rais Nicolás Maduro alijitangaza na kujiapiza kuwa mkuu wa nchi, katikati ya maandamano ya maelfu wanaopinga Serikali iliyopo madarakani. Alidai kuwa Katiba inamruhusu yeye kama kiongozi mkuu wa Bunge kuwa Rais wa mpito endapo uchaguzi utakuwa na mgogoro unaohitaji kuwa na Serikali ya mpito.
Marekani na washirika wake waliunga mkono hatua ya kujiapisha wakidai kuwa hawamtambui Maduro kama Rais wa nchi hiyo.
Hata hivyo, Urusi, China, Cuba, Uturuki na nchi nyingine washirika walipinga vikali hatua ya Marekani na kutangaza kumuunga mkono Rais Maduro.
Hivi karibuni, Rais Maduro alieleza kuwa Marekani inataka kufanya mapinduzi dhidi ya Serikali halali. Lakini alisema yuko tayari kufanya mazungumzo na upande wa upinzani.
“Niko tayari kukaa chini na upande wa upinzani tuzungumze kutafuta muafaka kwa maslahi ya Venezuela,” aliliambia shirika la habari la Urusi linalojukana kama RIA Novosti in Caracas.
Guaidó ameendelea kuwahamasisha wafuasi wake kuandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa Mei mwaka jana uliompa ushindi Maduro.