Raia wa Uchina, Lu Ke anayeshutumiwa kwa ubaguzi wa rangi na kuwanyanyasa watoto nchini Malawi ameshtakiwa kwa ulanguzi wa binadamu katika mji Mkuu nchi hiyo Lilongwe, Julai 18, 2022..
Raia huyo, Lu Ke (26), alikamatwa mwezi uliopita katika nchi jirani ya Zambia kwa kuingia kinyume cha sheria baada ya kutoroka Malawi wakati madai ya unyanyasaji dhidi yake yalipoibuka.
Ke, anadaiwa kuwarekodi watoto wakiimba nyimbo za ubaguzi wa rangi kwa lugha ya Kichina ambayo hawakuielewa, na kisha kuuza video hizo kwenye mitandao ya kijamii ya Jamhuri ya Uchina.
Mara baada ya kukamatwa, Ke alirejeshwa nchini Malawi na alifikishwa Mahakamani Julai 18, 2022 ambapo alishtakiwa kwa makosa matano ya kusafirisha watu ambapo Waendesha mashtaka wa Serikali wanasema mashtaka zaidi yanatarajiwa kufunguliwa uchunguzi utakapokamilika baada ya wiki mbili.
Hata hivyo, Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Lilongwe, James Mankhwazi alimnyima dhamana Ke akiteta hoja ya waendesha mashitaka walio onesha kuwa mshtakiwa anaweza kukimbia, kutokana na kutokuwa na mahali maalum pa kukaa na anaweza kuharibu uihahidi kwa kuwahadaa watoto hao.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali wa Malawi, Prescott Mwayiulipo naye alipinga Kortini suala la kumwachilia Ke kwa dhamana, akidai hatua hiyo itasaidia kumlinda dhidi ya watu waliokasirishwa na video hizo.
Katika taarifa yake ya mwezi jana, Ubalozi wa China nchini Malawi, ulilaani kitendo cha mshtakiwa na kusema Serikali ya China haiwezi kuvumilia vitendo vya ubaguzi wa rangi.