Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamisi Juma amewataka majaji nchini kuzingatia maadili ya taaluma yao na kutenda haki, kwa kuwa wana dhamana kubwa ya kusikiliza mashauri na kuyatolea uamuzi.
Jaji Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo elekezi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu Zanzibar, mafunzo yanayofanyika kwenye chuo cha uongozi wa mahakama (IJA) kilichopo Lushoto mkoani Tanga.
Amesema ni vema kwa Majaji hao wakazingatia miongozo ya taaluma yao, inayowasisitiza kutenda haki kwa jamii.
Mafunzo hayo elekezi yanashirikisha Majaji 31 na yanafanyika kwa muda wa siku saba.