Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo ifanye utafiti wa kina ili kupata aina bora ya mbegu za pamba zitakazowanufaisha wakulima.

Ameyasema hayo mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na wabunge wanaotoka katika mikoa inayolima pamba, ambapo amesema kuwa lazima Wizara ya Kilimo itumie taasisi zake vikiwemo vyuo kufanya uchunguzi na kubaini ni aina gani za mbegu zinafaa kutumika kulingana na eneo husika

“Mbegu za pamba ziko nyingi na zina migogoro. Mbegu nyingine zina manyoya, nyingine zina vipara hivyo lazima utafiti wa kina ufanyike ili kupata aina bora.”amesema Majaliwa

Amesema utafiti huo ambao utabainisha aina ya mbegu inayofaa kulingana na aina ya udongo katika kila eneo ili kumuwezesha mkulima kupata mazao ya kutosha.na kuweza kujipatia kipato kupitia kilimo.

Aidha, Majaliwa amewataka Maofisa kilimo kuhakikisha wanayasimamia vizuri mazao hayo ambayo ni korosho, chai, pamba, kahawa na tumbaku ili yawe na tija na kuleta matokeo chanya kwa wakulima.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Serikali inataka kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa zao la pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba, pembejeo hadi masoko ambayo yamekuwa ni changamoto kwa wakulima.

 

Kwa upande wake Mbunge wa Itilima, Njalu Silanga aliiomba Serikali izibane Halmashauri ili kuhakikisha fedha za miradi ya kilimo zinatumika ipasavyo.

Naye Mbunge wa Tarime Mjini, Bi Ester Matiko ameiomba Serikali kuwaelimisha wananchi na kuwahamasisha kulima kilimo hicho ili waachane na kilimo cha bangi.

 

Nyalandu: Nahitaji maombi yenu Watanzania
Jeshi la Zimbabwe lakanusha kufanya mapinduzi