Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa siku 30 kwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kujirekebisha na kumaliza tofauti zao ndani ya siku 30 na iwapo wataendelea na vurugu Serikali haitosita kuvunja baraza la Madiwani.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa mkoa wa Kigoma katika mkutano wa hadhara uliofanyika Manispaa ya Kigoma Ujiji kwenye uwanja wa Kawawa, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo.

Amefikia hatua hiyo mara baada ya Madiwani hao kutumia muda mwingi wakigombana badala ya kuwahudumia wananchi.

“Serikali hairidhishwi na utendaji wenu na nimewapa muda wa mwezi mmoja kumaliza tofauti zenu. Nataka muendelee kufanya kazi za kuwatumikia wananchi wa Manispaa hii ambao wamewachagua ili muwatatulie kero zao na si kuendeleza migogoro,” amesema Majaliwa

Amesema Madiwani hao wanatakiwa kufuatilia changamoto zinazowakabili wananchi wao ikiwemo ya upatikanaji wa dawa katika hospitali, zahanati na vituo vya afya, ambapo licha ya Serikali kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa lakini bado wananchi wanaendelea kukosa huduma hiyo.

Aidha, amesema kuwa matatizo ya madiwani wa Manispaa hiyo anayafahamu na iwapo watashindwa kujirekebisha Serikali haitosita kulivunja baraza hilo kwa sababu Madiwani wake wanatumia muda mwingi kugombana badala ya kuwahudumia wananchi.

Hata hivyo, Majaliwa amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Kigoma kwamba Serikali itaboresha miundombinu ya mkoa huo ikiwemo ya reli, barabara, ujenzi wa bandari na uwanja wa ndege utakaokuwa na uwezo wa kutua ndege kubwa.

 

Habari Picha: Rais Dkt Magufuli akiwafariji familia ya Eric Shigongo kwa msiba
Mourinho ang'aka baada ya kuchezea kichapo, ainyooshea kidole bodi