Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi wanaoshiriki katika ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wilaya ya Ruangwa kulinda fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kwa kuvitunza vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi ili mradi ukamilike kwa wakati.
Ametoa kauli hiyo leo (Juni 7, 2021) wakati alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika kijiji cha Nandagala wilayani Ruangwa, mkoa wa Lindi.
“Rais wetu anatupenda ndiyo maana katuletea pesa ambazo lazima tuzilinde, tukinunua vifaa vya ujenzi kama vile, mabati, saruji, mbao na nondo lazima vyote vitumike hapa kwenye ujenzi na kamwe tusiruhusu udokozi”
Waziri Mkuu amesema kuwa serikali itaendelea kuwaletea maendeleo wananchi na yeye akiwa mbunge wao anawajibika kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha Ruangwa inasonga mbele katika nyanja zote.
Pia Waziri Mkuu ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Uongozi wa VETA na Suma JKT kwa kusimamia kwa weledi na uaminifu ujenzi wa chuo hicho na amewataka kuhakikisha kwamba ujenzi unakamilika kwa wakati ili mafunzo yaanze kutolewa.
Akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema chuo hicho kitajengwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itagharimu shilingi bilioni 2.1 na awamu ya pili itagharimu shilingi bilioni 1.2.
Amesisitiza kuwa mafunzo ya muda mrefu katika chuo hicho yanatarajiwa kuanza mwenzi Januari 2022 kwa mujibu wa mafunzo ya VETA.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema kuwa Chuo kitakuwa ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa wakazi wa eneo la Nandagala na wilaya ya Ruangwa hivyo wazazi wawapeleke watoto wao wakajipatie maarifa na ujuzi