Serikali nchini, imesema inaendelea kufanya maboresho makubwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo hivi karibuni imetoa fedha kwa ajili kununua vifaa vya kisasa ikiwemo MRI inayoweza kumpima mgonjwa hata akiwa na chuma mwilini.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Desemba 23, 2022 mara baada ya kufanya ziara katika Hospitali hiyo na kisha kuzungumza na wagonjwa na wauguzi waliomemueleza kuwa huduma zinazotolewa hospitali hapo zinaridhisha.
Amesema, “Sambamba na huduma hizi nzuri zinazotolewa na wataalam wetu kwa moyo mkubwa Serikali inaendelea kufanya maboresho makubwa katika hospitali yetu ya Taifa ili iendelee kutoa huduma bora na za kisasa zaidi.”
Majaliwa amesema ameridhishwa na huduma zinazotolewa katika Hospitali hiyo na kuwapongeza watendaji wake kwa kuwahudumia wagonjwa kwa weledi na kuzungumzia suala la gharama kubwa za matibabu linalolalamikiwa wengi kuwa mpango wa bima ya afya kwa wote unakwenda kumaliza changamoto hiyo.
Aidha, Waziri Mkuu pia amewataka Watanzania ambao wanashindwa kumudu baadhi ya huduma za matibabu wawasilishe masuala yao katika ofisi ya Ustawi wa Jamii zilizopo kwenye hosptali husika, na watapewa maelekezo ya kufuata ili wapate msamaha.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Mohammed Janabi amewasisitiza wagonjwa wote ambao hawana uwezo wa kulipia huduma hizo mbalimbali zitolewazo hospitalini hapo wafuate taratibu watahudumiwa. “Kila mwezi hospitali inatoa msamaha wa zaidi ya shilingi bilioni moja kwa wasiokuwa na uwezo.”
Wakizungumzia kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wanaouguza ndugu zao katika hospitali hiyo wamesema huduma zitolewazo ni nzuri na hakuna anayeombwa rushwa ila changamoto waliyonayo ni juu ya matibabu yanatolewa kwa gharama kubwa.