Watu kadhaa wanaosadikika kuwa ni majambazi wamedaiwa kuteka kijiji cha Benako, wilayani Ngara mkonai Kagera kwa takribani saa mbili.

Taarifa kutoka kijini hapo zimeeleza kuwa watu hao waliokuwa wamejihami kwa bunduki na mabomu ya kurusha kwa mkono walifanya tukio hilo juzi majira ya saa mbili hadi saa nne usiku na kupora fedha taslimu shilingi milioni 4 pamoja na shilingi milioni 2.4 zilizokuwa kwenye simu (M-Pesa).

Majambazi hao wameripotiwa kumjeruhi mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Gankaga, Nelson Ismail aliyepigwa risasi pajani.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kagera, Abel Mtangwa alikanusha kutekwa kwa kijiji hicho na kueleza kuwa lilikuwa tukio la ujambazi tu.

“Naelekea katika eneo la tukio, lakini sio kweli kwamba majambazi yameteka kijiji,” alisema Kaimu Kamanda huyo wa Polisi. “Mwanafunzi aliyejeruhiwa kwenye paja la mguu wa kushoto amelazwa Hospitali Teule ya Omurugwanza na hali yake inaendelea vizuri,” aliongeza.

Alisema kuwa hadi jana hakuna mtu yeyote aliyekuwa amekamatwa kutokana na tukio hilo lakini kikosi kazi cha polisi kilipelekwa mpakani (Mwa Rwanda na Tanzania) kuwasaka watu hao.

 

 

 

 

DJ D Ommy, Millard Ayo, Harmonize watajwa kwa Mara ya Kwanza kuwania tuzo kubwa Marekani
Lowassa, Ole Sendeka, Ummy wamsindikiza Shelukindo