Na Lilian Mahena

Waswahili (Watu wanaoishi pwani ya Afrika Mashariki) husema mtaji wa kwanza wa mtu ni afya, na Afya humjenga mtu timamu zaidi.

Jana (Novemba 14), ilikuwa siku maalum ya maadhimisho ya ugonjwa wa kisukari duniani pamoja na uzito uliopita kiasi. Maadhimisho hayo huongozwa na taasisi ya kimataifa ya ‘International Diabetes Federation’ (IDF).

Kwa mujibu wa tafiti zilizowasilishwa katika maadhimisho hayo, zinaonesha kuwa ongezeko la watu mijini, mabadiliko ya mitindo ya maisha ikiwa ni pamoja mlo; na mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni mwa sababu za ongezeko la magonjwa ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa kisukari na magonjwa ya moyo. Unene uliopita kiasi huvuta magonjwa mengine.

Tafiti hizo zimeeleza kuwa, kwa watu wanaoishi Kusini mwa Jangwa la Sahara, nusu ya watu wanaoishi na ugonjwa wa kisukari ndio wanaofahamu kuwa wanaumwa ugonjwa huo. Hivyo nusu iliyobaki haifahamu wakati inatafunwa na ugonjwa huo. Hata hivyo, kwa wanaofahamu, ni mmoja tu kati ya kumi ambao wanahangaika kupata tiba mahsusi.

Unaweza kuona kuwa, watu wachache wamekuwa na utambuzi juu ya unene (uzito uliopita kiasi) na jinsi unavyoweza kusababisha mtu kupoteza maisha yake kupitia magonjwa nyemelezi. Kwa idadi ya wanaojua, imewasababisha kubuni mbinu mbalimbali za kuweza kuepukana na unene ikiwepo na kuanzisha makampuni ya kutengeneza dawa za kupunguza unene.

Video: Siri ya Masha kujitoa Chadema, ‘Bilionea’ wa nyumba za Lugumi aelezea alivyotekwa Urusi siku 28

Kampeni za dawa za kupunguza unene zimegeuka kuwa ‘dili’ na biashara kwa watu mbalimbali baada ya kubaini kuwa ni tatizo la dunia pia. Lakini dawa nyingi sio salama na hata zinazotajwa kuwa ni salama husababisha madhara kwa mtumiaji.

Unene uliopitiliza unasababisha magonjwa ambayo yapo kwenye orodha ya kwanza katika kuua watu duniani. Kutokana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) Magonjwa hayo ni  ugonjwa wa moyo, Kiharusi, shinikizo la damu pamoja na kisukari.

Unene uliopitiliza unasababishwa na ulaji mbovu wa chakula na kutokufanya mazoezi kabisa. Hivyo, kuufanya mwili kushindwa kuunguza mafuta mwilini na kupelekea mlundikano wa mafuta katika maeneo mbalimbali ya mwili ikiwemo tumboni na kuleta kitambi.

Kuna athari nyingi ambazo zinatokea kwa mtu aliye na unene uliopitiliza ambazo zinaweza kuleta shida katika maisha yake ikiwemo na mimba kuharibika kwa wanawake na kwa wanaume kupoteza uwezo wa kuzaa au upungufu wa nguvu za kiume, kupata uchovu uliopitiliza na kupenda kulala muda mwingi kitu ambacho kinaathiri hali ya kiuchumi pia.

Achana na dawa za kupunguza unene uliopitiliaza. Namna bora ya kuepukana na unene uliopitiliza ni kufanya mazoezi walau mara moja kwa siku ili kuchangamsha mwili. Mazoezi mazuri na ambayo hayahitaji kwenda sehemu za kufanyia mazoezi (gym) ni kukimbia, kuruka kamba, kuendesha baiskeli na kunyoosha viungo.

Ili kupata matokeo mazuri kwakufanya mazoezi unatakiwa kubadili mfumo wako wa ulaji. Yaani, kuacha kula chakula kingi wakati wa usiku na kula matunda kwa wingi. Kuna wanaofanya mazoezi kisha wanaongezeka badala ya kupungua, sababu ni kwamba wanafanya mazoezi sana na hivyo inawapa hamu ya kula na wanakula zaidi ya awali. Huwezi kupata matokeo unayoyataka kama hutarekebisha tabia ya kula.

Pia, kupenda kunywa maji kwa wingi badala ya soda na vitu vyenye sukari hasa isiyo asili, kuacha kabisa kula vyakula vyenye mafuta mengi.

Unene uliopitiliza si ugonjwa unaokuja bila mtu kujua bali mtu anaona jinsi anavyoongezeka hivyo unaweza kujiepusha na unene pamoja na madhara yake kabla hujafikia hatua mbaya kwa kubadilika sasa na kuchukua hatua.

Ili kuepuka kuwa kati ya orodha ya wenye matatizo yanayosababishwa na unene au ongezeko la uzito unaopitiliza, hakikisha unatokwa na jasho jinsi kwa kufanya mazoezi ili kuondoa sukari, mafuta na mengineyo na kuufanya mwili wako kuwa wenye afya zaidi.

Hata hivyo, mazoezi ya kweli sio kazi ndoto, inahitaji moyo na kujitoa kwani mwanzoni unaweza kupata maumivu kidogo ya mwili na uchovu. Usijaribu kuacha kwani waingereza wanasema ‘No Pain No Gain’.

 

Milioni 10 zatengwa kwa atakayetoa taarifa za kigogo wa PCCB
Mume wa Irene Uwoya afariki dunia