Wakati fulani, Wimbo wa DDC Mlimani Park Orchester uitwao HURUMA KWA WAGONJWA utunzi wake Shaban Dede ulipata kutamba sana, ukiwagusa wale wote wenye tabia ya kukwepa kuwasaidia wagonjwa na badala yake kuthamini misiba, kitu ambacho si kizuri.
Haikuishia hapo, Marehemu Huseein Jumbe naye alipata kuandika mashairi ya wimbo uitwao NANI KAIONA KESHO, ujumbe wake ukirandana kwa kiasi fulani na wa Dede katika kuwahimiza Ndugu, Jamaa na Marafiki kuweka utamaduni wa kuwajali watu wakati wa ugonjwa, na si katika misiba.
Tabia hizi ni za ajabu na hazina msaada, kwani zinafundisha umimi na kujitapa mbele ya kadamnasi ilhali wakati wa uhitaji wengi wetu tunakuwa nyuma sana kuleta matokeo yanayoacha alama, kwani watu humjali sana mtu akiwa marehemu kuliko akiwa hai.
Hili hujionesha wazi pale ambapo baadhi yetu tunagharamia misiba kwa nguvu na akili zetu zote huku tukionesha kuumizwa sana na waliotutoka kuliko kuokoa maisha yao walipokuwa wakiumwa, wala kwenda kuwajulia hali pale wanapougua, isipokuwa tunakodi magari tukijazana kwenda kuzika.
Wakati fulani niliwahi kuzungumza na Mzee Godfrey Makasi wa Kijiji cha Njoge, kilichopo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, yeye alisema maisha ni kubahatisha akimaanisha kuwa yeyote aliye bora kwa mwenzie katika maisha, basi amebahatika, akidai kuna muda huwa tunawaamini watu wasiopaswa kuaminiwa.
Alisema, “mwenye bahati habahatishi, bali ndivyo inavyompasa katika kufanikisha malengo yake, wangapi wana marafiki wasio na msaada wala kuwajali na wangapi wanafurahia uwepo wa marafiki wao na wakajivunia kabisa? hili ni jambo la kubahatisha na sisi tusio na bahati ikitokea umeshikwa shikamana.”
Nilimuelewa, kwani imekuwa ni nadra sana watu kukupa heshima ukiwa hai, lakini watapenda sana kukupa heshima za mwisho ukiwa kwenye Jeneza, kwa mfano unaweza kuwa hujawahi kupewa ua na mtu tangu uzaliwe, lakini ukifa watarundika maua mengi mno juu ya kaburi lako huku wakiwa na simanzi na wakionesha upendo wa hali ya juu.
Wengine hukesha msibani kwa ndugu au jirani yake aliyefariki au kufiwa, ila katika maisha ya uzima hukuwahi kufika ndani kwake hata siku moja, na wala hakuna anayetaka kujua kijiji unachotokea ila ukifa watajaa kwenye magari wasindikize jeneza lenye mwili wa marehemu, kitu ambacho ni chema lakini hakina afya.
RAFIKI HEWA NI YUPI?.
Mtambi na Chogeti ni marafiki wakubwa sana na jamii inatambua hivyo, lakini mfumo wa maisha ya kujiajiri uliwatenganisha, ila hilo halikuathiri mawasiliano yao ingawa ilitokea siku moja wakawa wanatumiana ujumbe wa maandishi kwa simu zao za mkononi wakijibizana kwa zamu.
Mtambi: Naumwa sana rafiki yangu Chogeti nimelazwa wiki ya pili sasa sina pesa kabisa.
Chogeti: Unaumwa nini Kaka?
Mtambi: Homa imenibana kweli aisee na naona pesa za kugharimia matibabu zinaniishia kabisa.
Chogeti: Ningekusaidia Bro. bahati mbaya kuna kiwanja tulipatana na muuzaji majuzi ndo nataka kesho nikanunue.
Mtambi: Sawa Kaka, ila siko vizuri kabisa kipesa nisaidie walau kidogo ndugu yangu.
Chogeti: Iko hivi, bajeti zote tunazopanga Mimi na Mke wangu, huwa hazivunjwi ndugu yangu. nimebakiwa na hiyo Milioni 5 tu ya kiwanja.
Mtambi: Ukinisaidia hata laki mbili tu inatosha rafiki yangu nikipona tu nitazirejesha.
Chogeti: Hapo itakuwa ngumu kidogo, na vipi umejaribu kuupigia Uongozi wa Chama chetu cha Wafanyabiashara?
Mtambi: Ndio, wamenichangia 30,000 tu kaka.
Chogeti: Anzia hata hiyo Bro. Get well soon.
Baada ya siku tatu mbele Mtambi alifariki kwani hakufanikiwa kupata msaada wa kumudu gharama za matibabu na hivyo kupelekea kukosa nguvu, ugonjwa kuzidi na mauti kumchukua hali iliyozusha taharuki kwa Ndugu, jamaa na marafiki ambao walianza kupeana taarifa kwa kasi ya ajabu, wakihimizana kufika msibani.
MATANGAZO MSIBANI.
Watu walipata nafasi ya kutoa machache ya moyoni huku rafiki wa marehemu Mtambi, Chogeti ambaye aliwasiliana naye akiombwa msaada akipewa umuhimu kutokana na ukaribu wao akipewa kinasa sauti na akasema,”Ndugu waombolezaji, Bwana Mtambi alikuwa rafiki yangu mkubwa tulioshibana, tuliyeshirikiana katika mambo mengi sana, hivyo Mimi kama Rafiki aliyekuwa zaidi ya Ndugu natoa mchango Milioni moja keshi.”
Chama cha Wafanyabiashara nao hawakuachwa nyuma, waliitwa na hii ilikuwa sehemu ya risala yao, “tumehuzunishwa sana na taarifa ya kifo cha Bw. Mtambi alikuwa Mtu muhimu sana kwenye chama chetu na ameacha pengo kubwa lisilozibika, sisi tutalipa gharama zote za hapa msibani, kuanzia chakula, usafiri hadi mazishi, asanteni.”
UJUMBE MUHIMU.
Ifikie kipindi tubadilike kwa kuanza kumthamini Mgonjwa kuliko Maiti, tunamuenzi sana marehemu kuliko alipokuwa Mgonjwa je, ni kwanini? tutambue kuwa kuthamini maiti (Marehemu), kuliko Mgonjwa ni unafiki mkubwa uliovuka viwango.
Huenda huyo mtu (mgonjwa), angesaidiwa kwa nguvu kubwa kama inayoonekana kwenye mazishi asingefariki na angepona kisha akawashukuru na MUNGU angewaandikia Thawabu na kuwamwagia baraka kwa shukrani za mtu aliyepona.
Tuwe na upendo, maana upendo ni neno linalotumika kwa maana mbalimbali kuanzia hali ya nafsi ya binadamu hadi kwa MUNGU, kama ambavyo C. S. Lewis katika kitabu chake cha “Four Loves” akiutaja upendo katika kona nne za maisha ya mtu, yaani maisha ya mtu kwa kuzingatia watu wa aina nne anaousiana nao.
Lewis anasema, “kuna aina nne za upendo ambazo ni, “upendo wa zawadi au uhitaji” (huu ni upendo wa mtoto kwa mama yake na upendo wa mama kwa mtoto wake, ni upendo kati ya mzazi na mtoto ambapo mtoto anampenda mama kutokana na uhitaji wake kwa mama, na mama anampenda mtoto kutokana na wajibu wake kama mzazi).”
Aidha, anaongeza kuwa aina ya pili ya upendo ni “storage” (huu ni upendo wa undugu, ndugu wa damu au ndugu wanaohusiana kwa namna moja au nyingine, ni upendo kati ya ndugu usiohusisha ngono au tendo la ndoa, watu wanapendana kwa kuwa ni ndugu).
Upendo mwingine ni “philia” huu ni upendo wa kirafiki unaotokana na wawili wasio ndugu kukaa pamoja na kushibana hata kuwa marafiki, “Eros” huu ni upendo unaohusisha ngono au tendo la ndoa, ni upendo kati ya mwanaume na mwaamke katika ndoa; na mwisho kabisa ni “agape” ambao ni upendo usiotegemea mazingira, upendo usio na masharti.
Lewis ameutaja upendo huu kuwa ni mkuu kuliko upendo wa aina nne uliotangulia kutajwa hapo juu na ni upendo ambao unapaswa kuwa msingi wa upendo wa aina yoyote ile jambo ambalo linanifanya niwape moyo wote waliowahi kukumbwa na madhila kama haya, kwa kuyashuhudia au yaliwahi kuwapata lakini MUNGU aliwaokoa na kifo, na hivyo wamebaki kustaaajabia na wamejifunza kushukuru kwa milango iliyofungwa katika maisha yao.
Hata hivyo, waelewe kuwa ipo milango ambayo unaweza kuingia kwa muda mchache lakini ikakuchukua maisha yako yote kuyaepuka madhara utakayoyapata kwa muda huo mchache ulioutumia kuingia na hivyo kuwa na majuto kwani wakati mwingine MUNGU hukuonyesha upendo wake kwa kufunga baadhi ya milango yako.
Yeye anajua wapi pa kukusaidia, na anajua alitaka akufunze nini na wewe upate uhalisia gani pengine hata kutambua aina ya marafiki waliokuzunguka kwasababu anajua kwamba iwapo akiruhusu ukaingia katika milango hiyo itakuharibia maisha yako yote kwani sio kila mlango uliofunguliwa ni mwema kwako.
“Mambo mengine au misaada mingine huweza kuonekana ni mizuri yenye faida na kuvutia lakini pindi tu unapoingia kwa kupewa misaada hiyo unaharibikiwa, unasimangwa, unanyanyaswa, unaaibishwa na hata kudharaulika kisa tu ulipata unafuu kupitia milango hiyo,” siku moja aliniambia rafiki yangu Thomas Mhozya.
Endelea kusali na kumuomba MUNGU, ili aweze kukuonyesha milango sahihi na hata pindi pindi unapoona baadhi ya milango imefungwa, usilaumu wala kunung’unika na badala yake mshukuru MUNGU na kumwomba akusaidie katika kutafuta njia sahihi zilizobeba fursa za baraka kwako.