Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amewataka Wananchi wote waliovamia na kujenga kwenye maeneo ya Mfuko wa hifadhi ya Jamii (NSSF), kutoa ushirikiano kwa mamlaka kwa kukubali kulipa fedha, ili waweze kumilikishwa maeneo hayo.
Makalla ametoa maelekezo hayo Kufuatia Kamati iliyoundwa kuchunguza mgogoro baina ya pande hizo mbili na uliobaini kuwa Wananchi hao walivamia maeneo ya NSSF na kujenga kinyume na sheria.
Aidha, Makala ameielekeza NSSF kurasimisha upya maeneo hayo kwa kupima Viwanja ili wavamizi walio tayari walipe na baada ya mgogoro kuisha Wananchi watapitiwa na zoezi la anuani za makazi liweze kuchukua nafasi yake.
“Maamuzi haya ni sehemu tu ya Busara ya Serikali na nitoe onyoa kwa Wananchi juu ya tabia ya kuvamia maeneo ya watu na Taasisi,” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Miongoni mwa Viwanja vya NSSF Vilivyovamiwa ni vya maeneo ya Mwapemba, Toangoma na Mtoni Kijichi huku eneo la Mwapemba lenye ukubwa wa Mita za mraba 210,000 likivamiwa na zaidi ya Wananchi 100 walioweka makazi yao ya kudumu.
Baadhi ya Wavamizi wa maeneo hayo akiwemo Rehema Mwita amemshukuru Makalla kwa uamuzi wa kuwaruhusu kulipa fidia, ili waweze kusalia katika eneo hilo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa NSSF Kulipa kiasi cha fedha kinachohitajiwa.