Waziri wa Nishati, Januari Makamba, yupo jijini Rotterdam, Uholanzi, katika Mkutano wa Viongozi wa Dunia unaojadili Program ya Afrika ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Africa Adaptation Summit), ulioanza hii leo Septemba 5, 2022.
Katika Mkutano huo, Waziri Makamba anamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ukilenga kushawishi Washirika wa Maendeleo, Taasisi za Kifedha na Sekta binafsi na marafiki wa Afrika kuchangia fedha kwenye Programu hiyo ya Afrika ambayo inahitaji Dola za Marekani Bilioni 25 ifikapo 2025.
Majaliwa ataka kasi na viwango kwa Wakandarasi wa barabara
Mmmoja wa washirika hao, Benki ya Maendeleo ya Afrika tayari imechangia Dola za Marekani bilioni 12.5 huku mkutano huo ukiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano wa 27 nchi wananchama wa mkataba wa mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba 2022 huko Sharm El Sheik nchini Misri.
Akiwa jijini Rotterdam, Waziri wa Nishati amekutana na Viongozi wa Dunia, Wakuu wa Taasisi na Mashirika mbalimbali na kujadiliana nao fursa mbalimbali ikiwa pamoja na namna bora ya Tanzania kunufaika na Mpango huo wa “AFRICA ADAPTATION ACCELERATION PROGRAM (AAAP).”
Mpango huo, unalenga harakisha mipango ya nchi katika kukabiliana na majanga yakiwemo UVIKO19, ukame, njaa, ajira kwa vijana na mafuriko huku suala la kuhimili mabadiko ya Tabianchi kwa Afrika ikiwa ni moja ya agenda muhimu ya mkutano huo.
Rais wa Jamhuri ya Senegal na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika pamoja Macky Sally, ndiye Mwenyekiti anayeongoza Mkutano huo kwa kushirikiana na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kituo cha kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (GCA), Ban Ki-Moon.