Waziri wa Nishati, Januari Makamba amezindua kiwanda cha kutengeneza transformer cha kampuni ya Elsewedy Electric kilichopo Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa kuhusu kiwanda hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Elsewedy Electric kwa Kanda ya Afrika Mashariki, Mhandisi Ibrahim Qamar amesema, ujenzi huo ni wa awamu ya pili na utawezesha kuzalisha transformer 2,500 kwa mwaka.
Amesema, “Transfoma hizo, zitakuwa ni kwa ajili ya soko la ndani pamoja na kuuza nchi za nje zaa Kenya, Madagascar, Rwanda, DRC, Zimbabwe na Afrika ya kusini.”
Ameongeza kuwa, kiwanda hicho kinatarajia kuajiri Watanzania zaidi ya 1,500 na kuwajengea uwezo vijana wanaomaliza vyuo pamoja na kujenga Chuo cha Ufundi.
Kufuatia hatua hiyo, Waziri Makamba ameipongeza Serikali ya Misri kupitia Balozi wake pamoja na uongozi wa Kampuni ya Elsewedy Electric, kwa ujenzi huo wa Awamu ya Pili.
Amesema, “Nawahakikishia soko la Transformer hizo kazi ya usambazaji umeme mijini, vijijini pamoja na vitongoji inaendelea na muongeze uzalishaji wa Transformer kwani katika kipindi cha miaka 5 kuanzia sasa zitahitajika Transformer 40,000 kwa ajili ya kupeleka umeme vitongojini.”
Aidha, Waziri Makamba amesema, “Transformer nyingine 50,000 zitakuwa ni kwa ajili ya Miradi ya TANESCO, Serikali inategemea kuwa bei ya Transformer hizo zitakuwa chini ikilinganishwa na bei ya ya Transformer zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.”
Hata hivyo, ameitaka Kampuni hiyo kuzalisha Transformer zenye uwezo mkubwa (Power Transformers), ambazo kwasasa zinaagizwa nje kwa gharama kubwa na huchukua muda mrefu kuwasili nchini.
Waziri Makamba, pia amemuhakikishia Balozi wa Misri na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Kampuni hiyo pamoja na Sekta binafsi kwa ujumla kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania.
Awamu ya kwanza ya ujenzi wa kiwanda hicho ilizinduliwa Desemba 2021 na Rais, Samia Suluhu Hassan, huku akisema kiwanda hicho pia kitazalisha vifaa vya umeme, vikiwemo Nyaya za umeme na mita.
Hafla hiyo ya uzinduzi, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa na Balozi wa Misri nchini Tanzania, Mohamed Jaber Abu El Wafaa.
Wengine ni Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Said.