Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda amewataka wananchi wa wilaya hiyo wanaoishi mabondeni kutii wito wa serikali wa kuondoka katika maeneo hayo ili kuepuka maafa yatakayotokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Makonda aliwataka wananchi waliogoma kuhama katika maeneo hayo ya Mabondeni kuhakikisha wanahama kwa hiari ili wasiilazimishe serikali kutumia nguvu.

“Hatupendi kutumia nguvu. Na mara nyingine watu tukitumia nguvu tunaonekana tuna jazba. Ninachowaomba wananchi wasilazimishe serikali ikatumia nguvu. Sehemu ambayo unajua kabisa ni hatari kwako, kwa kizazi chako na taifa lako tukubali (kuhama),”alisema Makonda.

Aliongeza kuwa tayari serikali imeshawapa maeneo baadhi ya watu lakini wamegoma kuhamia katika maeneo hayo huku wengine wakiyauza na kurudi tena mabondeni.

Mvua iliyonyesha jana katika jiji la Dar es Salaam kwa saa kadhaa ilizua kadhia kubwa na uharibifu wa mali na maafa kwa mifugo katika baadhi ya kaya jijini humo.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa maeneo ya mabondeni waliwaambia waandishi wa habari kuwa kamwe hawatahama katika maeneo hayo kama hawatapewa maeneo na kuhakikishiwa muendelezo wa maisha yao kiuchumi.

Homa ya Nguruwe yaibua taharuki Mwanza, Watu wakimbia ‘Kitimoto’
Mbowe azungumzia Kasi ya Magufuli, adai Hawako Tayari Kupinga Tu