Serikali nchini, imesema ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi umeongezeka katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 huku ikitumia zaidi ya shilingi Trilioni 19.46 kwa matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuendelea kwa ujenzi wa miradi ya kimkakati.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Bungeni jijini Dodoma, wakati akiahirisha mkutano wa kumi na kusema shilingi Trilioni 12. 29 zimepelekwa katika matumizi ya kawaida huku zaidi ya shilingi Trilioni 7 zikipelekwa katika shughuli za maendeleo.
Amesema, makusanyo hayo yanatokana na fedha za makusanyo ya ndani shilingi Trilioni 13.40 ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya shilingi Trilioni 11.68 sawa na asilimia 98 ya lengo la kukusanya kodi na kwamba makusanyo na utekelezaji wa miradi hiyo, katika kipindi hicho cha nusu mwaka uchumi wa Taifa umekua kwa asilimia 5.2.
Aidha, Majaliwa ameongeza kuwa upatikanaji wa fedha hizo umeiwezesha serikali kukamilisha masuala kadhaa ikiwa ni pamoja uendelezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), mradi wa Kufua Umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP), ujenzi wa mji wa Serikali Mtumba, kugharamia na kukamilisha zoezi la Sensa na uendelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi.