Beki wa kati wa klabu ya Liverpool, Mamadou Sakho ameondolewa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa, ambacho mwishoni mwa juma hili kitacheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya mabingwa wa dunia timu ya taifa ya Ujerumani.

Shirikisho la soka nchini Ufaransa FFF, limethibitisha taarifa za beki huyo kuondolewa kwenye kiksoi cha Didier Claude Deschamps jana jioni.

Sakho mwenye umri wa miaka 25, alipata majeraha ya goti, mwishoni mwa juma lililopita wakati wa mchezo wa ligi ya nchini England, ambapo Liverpool walikua nyumbani wakiwakabili Crystal Palace waliochomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja.

Vipimo vya awali vimeonyesha dhahir, Sakho hatoweza kuuwahi mchezo huo wa mwishoni mwa juma hili, na atahitaji mapumziko ya muda mrefu hadi atakaporejea kwenye hali yake ya kawaida.

Kufuatia maamuzi ya kuondolewa kwa Sakho kikosi cha Ufaransa, tayari kocha Didier Deschamps ameshafanya maamuzi ya kumuita beki wa klabu ya Saint-Etienne, Loic Perrin.

Timu ya taifa ya Ufaransa, pia itacheza mchezo wa kirafiki kati kati ya juma lijalo dhidi ya timu ya taifa ya England kwenye uwanja wa Wembley.

Taifa Stars Kurejea Nyumbani Kesho
Zitto Kabwe Ampa Rais Magufuli Ushauri Mgumu