Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City wamepanga kuwakomoa Arsenal kuhakikisha wanambakiza kiungo Ilkay Gundogan kwa kufanya kila wanaloweza kumshawishi asaini mkataba mpya huko Etihad.
Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta anataka kuungana tena na Gundogan baada ya kuwahi kuwa pamoja wakati alipokuwa msaidizi wa Pep Guardiola huko Man City kabla ya kwenda kuwa kocha Emirates.
Mkataba wa Gundogan huko Man City utafika tamati mwishoni mwa msimu huu na mazungumzo ya mkataba mpya yameshindwa kufikia mwafaka. Barcelona wameonyesha dhamira ya dhati ya kuhitaji saini yake na wamempa ofa ya mkataba wa miaka miwili kwa ofa ya mshahara uleule kama anaolipwa kwenye klabu yake ya sasa ya Man City.
Jambo hilo limewafanya Arsenal kufikiria kwenda kumchukua Gondogan ili kwenda kumalizia mahali walipokwama kwenye kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya msimu huu kukosa kidogo. Lakini, Man City kwa sasa mpango wao ni kumfanya Gundogan kuendelea kubaki Etihad.
Kama atabaki basi jambo hilo litakuwa na faida kubwa kwa Man City na pigo kubwa kwa Arsenal ambao wanaamini wangewashinda Barcelona katika mbio za kunasa huduma ya supastaa huyo wa Kijerumani.
Gundogan alifunga mara mbili katika mechi zote mbili za mwisho alizoanzishwa dhidi ya Leeds United na Everton na kuifanya Man City kuwa kwenye nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa kabla ya kuwachapa Chelsea na kunyanyua taji hilo.