Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC Murtaza Mangungu amewashukia baadhi ya Waadhishi wa Habari, kwa kusema wamekua chanzo cha chokochoko za kuibua migogoro ndani ya Klabu hiyo, kwa kigezo cha matokeo ya hivi karibuni.
Simba SC imeshindwa kupata alama tatu katika michezo mitatu mfululizo, miwili ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Horoya AC na Raja Casablanca na mmoja wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC.
Mangungu amefunguka hayo alipohojiwa na E FM Radio katika kipindi cha Sports Head Quarter mapema leo Alhamis (Februari 23), kufuatia baadhi ya Waandishi wa Habari kutilia mkazi maoni ya Mashabiki wanaodai, kiongozi huyo hakushinda Uchaguzi uliofanyika Januari 29-2023.
“Huyo anayepinga matokeo ya Uchaguzi anakosea. Taratibu za Uchaguzi zilifayika.”
“Kama mtu hajaridhika na matokeo anajua cha kufanya. Ninachofahamu haki ya kugombea iko kwa mtu mmoja. Hao wanaopinga matokeo ni kina nani? Si watajwe majina yao tuwajue.”
“Waandishi wa Habari kwa kiasi mnataka kuwa chanzo cha kuleta matatizo. Haya mnayoyafanya ni kuchochea migogoro katika vilabu. Niko tayari kumsikiliza kila mtu ambaye atakuja ofisini.” amesema Mangungu
Mangungu alitangazwa kuwa Mwenyekiti wa Simba SC kwa ushindi wa Kura 1311 dhidi ya mpinzani wake Adv. Moses Kaluwa aliyepata kura 1045.
Kwa ushindi huo Mangungu alipata wasaa wa kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Simba SC kwa kipindi cha miaka minne ijayo, baada ya kuiongoza Klabu hiyo kwa miaka miwili tangu 2021.
Kwa upande wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi walioshinda ni Dr Seif Ramadhan Muba (1636), Asha Baraka (1564), CPA Issa Masoud Iddi (1285), Rodney Chiduo (1267) na Seleman Harubu (1250).
Jumla ya Wanachama Simba SC waliopiga Kura ni 2363 Kura halali, lakini Kura halali zilikuwa 2356.