Uongozi wa Simba SC umeendelea kusisitiza kuwa na imani kubwa na Kocha Mkuu wa kikosi chao Roberto Oliviera ‘Robertinho’ katika mpango mkakati wa kufikia malengo yao msimu huu.

Simba SC jana Jumatano (Februari 22), ilitoa taarifa rasmi ya kuendelea kufanya kazi na Kocha huyo kutoka nchini Brazil, kupitia kurasa za Mitandao ya Kijamii, ikikanusha uzushi uliokuwa umesambaa mitandaoni.

Akizungumza na Wasafi FM mapema leo Alhamis (Februari 23) Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema, Kocha Robertinho ataendelea kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi la klabu hiyo.

Ahmed amesema, Uongozi unaridhishwa na anachokifanya Kocha huyo mwenye umri wa miaka 62, na kwa sasa ni mapema mno kuanza kumuhukumu.

“Uongozi unaridhishwa mno na kile anachokifanya Robertinho.Kwa sasa ni mapema mno kuanza kumhukumu. Tunashirikiana naye vizuri,tunamuamini na bado ataendelea kuwa sana Simba”. amesema Ahmed Ally

Uzushi wa kutimuliwa kwa Kocha Robertinho ulianza kusambazwa katika Mitandao ya Kijamii saa chache baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, uliomalizika kwa sare ya 1-1 juzi Jumanne (Februari 21).

Robertinho aliajiriwa Simba SC Januari 03-2023, akitokea Vipers SC ya Uganda ambayo aliipa mafanikio makubwa msimu uliopita, kwa kutwaa taji la Uganda na Kombe la Shirikisho nchini humo, huku akiifikisha Hatu ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuitoa TP Mazembe ya DR Congo.

Mchungaji aomba radhi kwa kuhubiri na silaha madhabahuni
Francis Baraza aipeleka Simba SC Robo Fainali