Hali ya usalama ya eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), inaendelea kuzorota ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), linasema kati ya mwezi Februari – Juni 2022, zaidi ya watu 800 wameuawa katika mashambulizi ya kujihami.
Msemaji wa shirika hilo, Matthew Saltmarch amesema, “tunasikitishwa na tuna wasiwasi mkubwa kutokana na idadi kubwa ya vifo na machungu ya raia ikiwemo raia kulazimishwa kukimbia makwao kutokana na mashambulizi ya kikatili kwenye majimbo ya Mashariki mwa DRC.”
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo Saltmarch amesema, majimbo hayo ni ya Kivu Kusini na Ituri ambapo amedai kuwa hali hiyo isiyovumilika inaendelea kukua na katu haipaswi kuendelea kupuuzwa.
Amesema, “mwezi huu pekee mashambulizi ya mfululizo kutoka waasi jimboni Ituri yamesababisha vifo vya watu 11 na nyumba 250 kuporwa mali na kisha kuteketezwa moto. Na Kati ya Februari na Juni mwaka huu UNHCR na wadau wamerekodi zaidi ya vifo vya watu 800 kutokana na mashambulizi ya kutumia silaha na mapanga kwenye jamii mbalimbali jimboni Ituri.”
Aidha, ameongeza kuwa takribani ya watu 715 kati ya hao waliokufa walikuwa wamesaka hifadhi kwenye maeneo ya wakimbizi wa ndani au waliuawa wakati wanarejea nyumbani baada ya kukimbia ghasia.
Zaidi ya watu 20,700 wamekimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ambayo pia yamechochea uhaba wa chakula jimboni Ituri ambalo lina rutuba kubwa huku likiwa halina maendeleo kutokana na miongo kadhaa ya mapigano ya kikabila na hivyo kukosesha familia mbinu za kipato.
Jimboni Kivu Kaskazini, makazi ya wakimbizi wa ndani ya Kashuga yaliyoko mjini Masisi yalisambaratishwa mwezi Juni baada ya watu waliojihami kuvamia na kuua watu wanane na wengine saba walijeruhiwa.
Saltmarsh amesema, katika wiki za karibuni mapigano kati ye jeshi la DRC, (FARDC) na waasi wa kikundi cha M23 jimboni Kivu Kaskazini yamewakimbiza watu zaidi ya 160,000 kwenye maeneo ya Rutshuru na Nyiragongo.
“Kupangwa upya kwa jeshi la serikali kwenye mzozo huu kumejenga ombo la mamlaka na utete wa usalama kwenye majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini. Mashambulizi yaliyoratibiwa vyema na vikundi vya wanamgambo vilivyojihami vinanyanyasa raia kila uchao majimbo ya mashariki,” amesisitiza msemaji huyo.
Amefafanua kuwa, mashambulizi ya kila uchao yanakwamisha operesheni za UNHCR kufikisha misaada kwa jamii zilizo hatarini wakati huu ambapo ombi la shirika hilo la usaidizi kwa DRC limefadhiliwa kwa asilimia 19 pekee kati ya dola milioni 225 zinazohitajika.
“Tunatoa wito kwa wadau wote kukomesha ghasia hizi zisizo na maana ambazo zinalazimu watu kukimbia makwao. Tunatoa wito wa kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu na za usaidizi wa kibinadamu,” amesisitiza Saltmarsh.
Zaidi ya watu milioni 5.6 nchini DRC ni wakimbizi wa ndani na hivyo kufanya idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani siyo tu barani Afrika bali na Duniani kiujumla.